Wajumbe wa Kikosi kazi maalum kilichoandaa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, wakisikiliza kwa makini maoni ya wadau kuhusu mpango huo ili kuuboresha kabla ya uzinduzi wake jijini Dodoma.
Miongoni mwa wadau walioshiriki Mkutano wa kusanya maoni ya kuboresha Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, wakimsikiliza kwa makini mwezeshaji (hayupo pichani) alikuwa akiwapitisha katika mpango ulioandaliwa kwa ajili ya maboresho jijini Dodoma.
Mwezeshaji kutoka Kikosi kazi maalum kilichoandaa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, Bw. Shani Mayosa akiwapitisha wadau (hawapo pichani) katika Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha jijini Dodoma .
Mwalimu wa Vikoba, Bw. Evance Chipindi akitoa maoni katika mkutano wa Wizara ya Fedha na Mipango na baadhi ya wadau wa Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha wa kukusanya maoni ya kuboresha Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha jijini Dodoma.
Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini kutoka Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania, Bw. Mwombeki Baregu ambaye pia ni miongoni mwa wajumbe wa Kikosi kazi maalum kilichoandaa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, akifafanua jambo wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya kuboresha Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, Jijini Dodoma.
Msimamizi wa vikundi vya kifedha kukuza maendeleo ya Wahadzabe, Bw. Jacobo Lubumba akitoa maoni yake kuhusu Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha katika mkutano wa kukusanya maoni ya kuboresha Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha jijini Dodoma.
……………………
Na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Wizara ya Fedha na Mipango imekutana na baadhi ya wadau wa Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha kwa ajili ya kujadili na kupata maoni ya namna bora ya kufikisha elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma, Afisa Mwandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Janeth Hiza ameleeza kuwa Wizara imeandaa mkutano huo kwa ajili kukusanya maoni ya wadau mbalimbali ili kuona namna bora ya kufikisha elimu kuhusu umuhimu wa Sera na Sheria hiyo kwa wananchi wote.
“Mpango huu umetokana na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 ambayo imeanza kutumika rasmi Novemba 1, 2019 baada ya kutangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango katika gazeti la Serikali”, alisema.
Alisema Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) waliunda kikosi kazi kwa ajili ya kuandaa Mpango wa kutoa Elimu kwa Umma kuhusu Sera na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ambao upo katika hatua za mwisho za kuanza utekelezaji wake.
Bi. Hiza aliongeza kuwa maoni ya wadau hao yataiwezesha Wizara kujua namna bora ya kuwafikia wadau wote muhimu kwa urahisi kwa kujadiliana nyenzo na namna ya uwasilishwaji wake ambazo zitawawezesha wananchi kuelewa na kutekeleza matakwa ya Sheria hiyo.
Bi. Hiza alisema mkutano huo wa kukusanya maoni, makundi yote muhimu yamehusishwa wakiwemo vijana, wanawake, walemavu, walimu wa vikundi vya kifedha na wahamasishaji.
“Makundi yote tuliyokutana nayo yametoa maoni mazuri, wametuongezea mbinu mbalimbali ambazo tunaahidi kuzitumia katika mchakato huu wa kuwawezesha wananchi kupata elimu hii ambayo inalenga kukuza Sekta ya huduma ndogo za fedha nchini”, aliesema.
Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini kutoka Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Bw. Mwombeki Baregu alisema mkutano huo ni muhimu na umefanyika wakati muafaka ambao Sheria imeshaanza kutumika.
Alisema baada ya maoni hayo kufanyiwa kazi, Wizara ya Fedha na Mipango itatoa utaratibu wa kuzindua mpango huo wa Elimu kwa umma ili uanze kutekelezwa rasmi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Bw. Shani Mayosa ambaye pia ni miongoni mwa wajumbe wa kikosi kazi kilichoandaa mpango huo, alisema lengo kuu la Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ni kuwalinda watumiaji na watoa huduma hizo kisheria.
Alisema Sheria imeweka utaratibu wa kuwatambua watumiaji na watoa huduma ndogo za fedha ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza kipindi cha nyuma wakati Sheria hiyo haipo.
Aidha, wadau mbalimbali walioshiriki mkutano huo wameipongeza Serikali kwa kuandaa mpango huo na kuahidi kuusubiri kwa shauku kubwa kwa kuwa utaweza kujibu maswali mengi waliyokuwa wakijiuliza kuhusu kutungwa kwa Sheria hiyo ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2019.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Bidii, Bi. Esther Nkambwe, ambaye ni miongoni mwa wadau walioshiriki katika semina hiyo, alisema kuanza kutekelezwa kwa mpango huo wa elimu utaleta ahueni kwa wananchi ambao walianza kupata hofu kwa kudhani kuwa Sheria hiyo imekuja kuvisambaratisha vikundi.
Alisema mpango wa elimu utakapozinduliwa wananchi watapata ufahamu mzuri kuhusu Sheria hii ambayo ni msaada mkubwa katika Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha nchini.