Home Mchanganyiko MADIWANI MANISPAA YA IRINGA KUWEKA MKAKAKATI WA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA

MADIWANI MANISPAA YA IRINGA KUWEKA MKAKAKATI WA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA

0

Diwani wa kata ya Kihesa Juli Sawani (kulia) akiteta jambo na diwani wa kata ya Mwangata Nguvu Chengula leo wakati wa kikao cha baraza la madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa

Mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Alex Kimbe akifunga kikao cha baraza la madiwani leo ,kulia ni mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Hamid Njovu na kushoto ni naibu meya Joseph Ryata

…………………………

Na Francis Godwin,Iringa

Baraza la madiwani la halmashauri ya Manispaa ya Iringa limeanza kujipanga kutotua changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi waliofaulu mtihani wa Taifa wa darasa la sababu ambao wanapaswa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani 2020 .

Wakizungumza leo mara baada ya taarifa ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Hamid Njovu aliyoitoa kwenye kikao cha baraza la madiwani juu ya hofu ya wanafunzi kukosa nafasi katika baadhi ya shule za sekondari kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari mjini hapa ,madiwani hao walisema wameanza kujipanga kujenga vyumba vya madarasa .

Diwani wa kata ya Mwangata Nguvu Chengula na diwani wa kata ya Kitwiru Baraka Kimata walisema kuwa kwenye kata zao wamejipanga kukabiliana na tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa kweye shule za sekondari zilizopo ili kuwezesha watoto hao kuanza masomo ya sekondari kwa wakati .

Chengula alisema katika kata yake ya Mwangata kuna shule moja pekee ya sekondari ambayo ina kidato cha kwanza hadi cha sita na kuwa upungufu wa madarasa ni vyumba vinne japo upungufu huo hautazuia wanafunzi wa kidato cha kwanza kukosa nafasi ya kujiunga na shule hiyo mwakani .

Kwani alisema upungufu huo hautazuia wanafunzi wapya kujiunga na kidato cha kwanza kwani kuna vyuba ambavyo vipo wazi baada ya kidato cha nne kuondoka shule hapo.

“Baada ya wanafunzi wa kidato cha nne kuhitimu kuna vyumba kama vitatu vimebaki wazi ambavyo vitaweza kusaidia kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani 2020, mwaka 2019 shule hii ya Mawerewere ilikuwa na ukosefu wa chumba kimoja cha darasa ila mwaka huu kutokana na ufuaulu mkubwa wa watoto wa darasa la saba kumekuwepo na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa “

Diwani wakata ya Kitwiru Baraka Kimata alisema kuwa kata yake kuna upungufu wa vyumba 10 vya madarasa na kuwa tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa limekuwa ni kubwa kila mwaka jambo ambalo linahitaji mkakati wa kutatua tatizo hilo ili lisiendelee kuwa wimbo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa .

“Changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na kuwa ni changamoto ila kwa sehemu nyingine ni mafanikio kwani kuongezeka kwa watoto kwenda shule na sera ya elimu bila malipo iliyoanzishwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli ndio ambayo imeongeza kasi ya wazazi kusomesha watoto na hivyo njia pekee ni kuendelea kwenda na kasi hiyo kwa kuongeza shule Zaidi ya sekondari “ alisema Kimata

Hata hivyo alisema haungi mkono kwa ujenzi wa shule mpya unaoanzishwa katika ukanda wa Mwangata kwa mstahiki meya Alex Kimbe (CHADEMA) kuwa unafanyika kisiasa Zaidi kwani hakuna haja ya kuanzisha shule mpya za sekondari wakati kuna shule kongwe ambazo zinachangamoto ya vyumba vya madarasa hivyo badala ya kuanzisha ujenzi mpya walipaswa kuongeza ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule kongwe kama Mawerewere na nyingine .

Kimata alisema katika kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa kwenye kata ya Kitwiru ameanza mkakati wa kuongeza vyumba vya madarasa Zaidi na anaendelea kuwaomba wananchi na wadau kuunga mkono jitihada za ujenzi wa vyumba vya madarasa ili watoto wote watakaochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari mwakani .

Naibu meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Joseph Ryata alisema kuwa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto vya vyumba vya madarasa ,Halmashauri ya Manispaa hiyo imenunua mashine za kufyatua tofali ili kusaidia kuharakisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule mbali mbali za sekondari .

Pia alisema wameandaa mkakati wa kukutana na wadau wa maendeleo Manispaa ya Iringa ili kusaidia kunusuru tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa ili Januari mwaka 2020 watoto wote waweze kuingia darasani .

Awali mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Njovu alisema shule ya sekondari Tagamenda ina upungufu wa madarasa 10 hivyo haitaweza kupokea wanafunzi wapya mwakani,shule ya sekondari Ipogolo inakabiliwa na upungufu wa madarasa sita wakati Kihesa inakabiliwa na upungufu wa madarasa 12 hivyo shule hizo hazitapokea wanafunzi mwakani .

Mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Kimbe pamoja na kupongeza Halmashauri hiyo kwa kuongoza kimkoa katika ufaulu wa mitihani wa darasa la saba bado alitaka jitihada mbali mbali ziendelee ili kuwezesha wanafunzi wote waliofaulu wanakwenda sekondari .

Wakati huo huo diwani wa kata ya Gangilonga Leonard Mgina ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na waziri mkuu Kassim Majaliwa wakati wa ziara yake mkoani Iringa kutaka Halmashauri kupitia makusanyo yake ya ndani kuangalia uwezekano wa kutumia fedha katika kuboresha miundo mbinu ya barabara ili kuondoa changamoto ya barabara mjini hapa .

Alisema kuwa Halmashauri kupitia makusanyo yake ya mapato inauwezo wa kujenga barabara za kiwango cha lami ili kukuza uchumi Halmashauri kwani vijana wa babaji wanafanya kazi katika mazingira magumu kupitia barabara mbovu .

Mgina alisema kwa kata yake ya Gangilonga anapongeza wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) kwa kukusudia kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami katika barabara ya Mama Siyovelwa hadi Sambara ambayo itasaidia kupunguza changamoto ya barabara kwa madereva bajaji mjini hapa .