Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango akizungumza wakati akifungua mkutano wa uliokutanosha mabenki na Benki Kuu ya Tanzania BoT unaofanyika kwenye ukumbi wa BoT jijini Dar es salaam.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga akizungumza katika mkutano huo uliofanyika leo katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania BoT jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabenki (TBA) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa shukurani zake kwa serikali na Benki Kuu ya Tanzania BoT kwa usimamizi wake mzuri kwa taasisi za fedha nchini.
Baadhi ya washiriki wa mkutan huo wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi za kifedha na mabenki.
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango amesema sekta ya fedha
imekua na kuimarika, licha ya changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa
zikijitokeza huku akitaja mambo nane ambayo yanastahili kuzatamwa kwa kina
katika sekta hiyo.
Dk.Mpango amesema hayo leo Novemba 21,2019 wakati akifungua mkutano
mkuu wa 19 wa sekta ya fedha nchini.Dk.Mpango amefungua mkutano huo kwa
niaba ya Rais Dk.John Magufuli.
“Napenda niwapongeze kwa dhati wadau wote wa sekta ya fedha kwa mafanikio
makubwa yaliyofikiwa hadi sasa. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
ameyaainisha vizuri, nitaomba nijielekeze kuwaomba washiriki wa kongamano
hili watusaidie mawazo na mikakati ya kupiga hatua zaidi katika maeneo
yafuatayo,”amesema.
Dk.Mpango amesema kwanza amewaomba watumie fursa hiyo kujadili kwa kina
namna bora itakayowezesha taasisi za fedha kuwafikia wananchi wengi wa vijijini
kwa gharama nafuu. Takriban asilimia 66 ya Watanzania wanaishi vijijini kwa
kutegemea kilimo ambacho ndiyo chanzo kikuu cha kukidhi mahitaji ya chakula
nchini na malighafi kwa ajili ya viwanda.
“Hali halisi ni kuwa wengi wao bado hawajafikiwa na huduma za fedha (ikiwemo
mikopo),”amesema Dk.Mpango.
Amesema pili ni eneo la riba za mikopo bado ziko juu kiasi kwamba watu wengi
wanashindwa kukopa na baadhi ya waliokopa kushindwa kurejesha. Hivyo, licha
ya juhudi za kuboresha sekta hiyo ambazo Gavana amezisema,ameomba wadau
wa sekta hiyo watoe mapendekezo ya mikakati ya kushusha riba ili kuwezesha
upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu na hivyo kuchochea maendeleo ya
uchumi. Itafaa kongamano hilo libainishe mikakati mipya ya kupunguza na
kudhibiti kiasi cha mikopo chechefu katika mabenki.
Wakati jambo la tatu ni kwamba mikopo kwa sekta ya kilimo bado siyo ya
kuridhisha, kwani imekuwa ikipokea chini ya asilimia 5 ya mikopo yote itolewayo
na mabenki. Sekta hiyo imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.3 kwa
kipindi cha miaka 4 iliyopita ikilinganishwa na matarajio ya Serikali ya ukuaji wa
asilimia 13.1 ifikapo 2025.
” Sekta ya kilimo ni muhimu siyo tu katika kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda,
lakini pia kama nilivyokwisha sema ndiyo chanzo kikuu cha chakula na fursa za
ajira kwa Watanzania walio wengi, lakini pia ndiyo sekta yenye uwezo wa
kupunguza umaskini na kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa kiasi
kikubwa.
“Hivyo, ni matarajio yangu kuwa mjadala wenu utaangalia namna bora ya
kuzifanya taasisi za fedha kuongeza mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kilimo cha
mazao, ufugaji, uvuvi na biashara husika,”amesema Dk.Mpango.
Pia ameungana na Gavana kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali na
wadau mbalimbali kuboresha sekta ya fedha, ikiwemo kujenga Kanzidata za
taarifa za wateja na utoaji wa vitambulisho vya Taifa.
Hata hivyo ametoa rai kwa Mamlaka husika kuharakisha utoaji wa vitambulisho
vya Taifa kwa upande mmoja na mabenki kwa upande wao kuhakikisha
yanaboresha utoaji wa huduma za kifedha.
Dk.Mpango amesema jambo la tano ni kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa
miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway)
ambayo itarahisisha usafirishaji na uchukuzi.
Pia ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maji kwenye mto Rufiji
(2,115 MW) na maboresho ya sekta ya anga. Miradi hiyo inahitaji fedha nyingi
kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani na nje.
“Hivyo, ni matarajio yangu mkutano huu utajadili na kutoa mapendekezo ya
namna taasisi za fedha zinavyoweza kuchangia katika upatikanaji wa fedha za
kugharamia miradi hii ya kimkakati na ile ya sekta binafsi,”amesema.
Wakati jambo la sita ni kuhusu umuhimu wa sekta ya fedha katika ulipaji wa
kodi. Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani, wastani wa
makusanyo ya kodi kwa mwezi yalikuwa Sh. bilioni 850, lakini sasa ni wastani
wa Sh.trilioni 1.3.
“Kwa miezi ya hivi karibuni tumekuwa tukikusanya wastani wa zaidi ya Sh.trilioni
1.5 kuanzia Julai hadi Oktoba 2019. Pamoja na kwamba sekta ya fedha imekuwa
miongoni mwa walipa kodi wazuri.
“Napenda nitoe mwito kwa taasisi hizi kuendelea kushirikiana na Serikali katika
kuboresha mifumo ya malipo ya ukusanyaji wa kodi. Na kwa misisitizo, ni
muhimu hili iendane na matumizi ya kielektroniki katika kufanya
miamala,”amesema.
Dk.Mpango amewakumbusha wadau hao kuwa kuna Mpango wa Taifa wa
Kuboresha Mazingira ya Biashara na Mpangokazi wa utekelezaji wake
umeshakamilika. Hivyo ametoa mwito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na sekta
ya fedha kushiriki kutekeleza Mpangokazi huo ili kuboresha mazingira ya
biashara na uwekezaji.
“Nawakumbusha kuwa sekta ya fedha ina mchango mkubwa sana katika
kufanikisha Mpangokazi huo. Nane, natambua sekta isiyo rasmi nchini bado ni
kubwa na haipati fursa ya kutosha kunufaika na huduma rasmi za kifedha.
“Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kurasimisha rasilimali na
biashara, ikiwa ni pamoja na utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara
wadogo wadogo (wamachinga),”amesema Dk.Mpango.
Ameongeza lengo ni kuwawezesha wajasiriliamali hao kuingia kwenye mfumo
rasmi ili waweze kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi. Natoa
changamoto kwenu Taasisi za Fedha kuhakikisha kuwa mnatoa huduma ambazo
zitawawezesha walio katika sekta isiyo rasmi kujumuishwa katika mfumo rasmi
wa fedha.
Aidha, amesema wadau wote wa sekta ya fedha chini ya uongozi wa Benki Kuu
na Wizara ya Fedha washirikiane kuweka mazingira mazuri ya taasisi za fedha
kuwafikia wale walio katika sekta isiyo rasmi.