Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Cheptoo Amos Kipronoh (hayupo pichani) kuweka katika vipaumbele vya Benki hiyo kwa Tanzania kuhusu ujenzi wa Barabara ya Morogoro Dodoma yenye upana wa njia nne, kulia ni Kamishna Msaidizi wa Bajeti Bw. Emmanuel Tutuba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Cheptoo Amos Kipronoh, akieleza nia ya Benki yake ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato Jijini Dodoma, wakati wa Mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Amos Cheptoo, baada ya mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa nne kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Amos Cheptoo, (wa nne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa waandamizi wa Wizara hiyo na Benki ya AfDB , Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Amos Cheptoo, wakiwa katika Mkutano Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango)
***********************************
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika kuipatia Tanzania mkopo nafuu kwa ajii ya kujenga barabara ya njia Nne kuanzia Morogoro hadi Dodoma ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo
Dkt. Mpango ametoa ombi hili Jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo anayewakilisha nchi nane za ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Amos Cheptoo.
“Barabara hii ilijengwa muda mrefu miaka ya 80, malori mengi yanapita hapa kwenda Mwanza, Kigoma na nje ya nchi ikiwemo Burundi, Rwanda, na unaona kabisa imeelemewa na imeanza kuharibika” Alisema Dkt. Mpango
Alisema amemwomba Mkurugenzi Mtendaji huyo wa AfDB waanze kuliweka jambo hili kwenye miradi itakayogharimiwa na Benki hiyo baadae ili barabara hiyo itakayo kuwa na uwezo wa kuelekeza magari mawili kwenda upande mmoja na mengine mawili kupita upande mwingine iweze kujengwa.
“Baada ya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi, tunahitaji usafirishaji kwa njia ya barabara uwe na tija zaidi, uende haraka zaidi lakini pia kupunguza ajali. Hivi sasa kuna ajali nyingi sana kwa sababu magari yanayokwenda Dar es Salaam na yanayokuja Dodoma au kwenda Mwanza yanapishana kwenye haka kanjia kamoja” alisisitiza Dkt. Mpango
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Bw. Amos Cheptoo aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, alisema Benki yake itahakikisha Tanzania inapata mikopo ya miradi yake ya kimkakati na ya kipaumbele ukiwemo huo wa barabara ya Morogoro hadi Dodoma.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Cheptoo Amos Kipronoh, ameitaka Sekta Binafsi nchini Tanzania kuchangamkia fursa za mikopo nafuu zilizopo katika Benki hiyo.
Bw. Kipronoh alisema kuwa Sekta Binafsi nchini Tanzania ina nafasi nzuri ya kupata mikopo na utaalam utakaoiwezesha kujikwamua kiuchumi kwa lengo la kutokomeza umasikini katika Bara la Afrika.
“Sekta Binafsi hapa Tanzania haijatumia vizuri dirisha la mikopo ya Sekta hiyo ikilinganishwa nan chi nyingine za ukanda huu wa Afrika na ninakuomba Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango uihamasishe Sekta Binafsi ikope fedha hizo ili kukuza mitaji yao na kuongeza tija” alisema Bw. Cheptoo
Aidha, alisema kuwa Benki ya AfDB ipo katika hatua za mwisho za kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato Dodoma na tayari benki hiyo imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko mjini Dodoma pamoja na miradi mipya ya kuzalisha Nishati ya umeme ambayo iko mbioni kuwasilishwa katika vikao vya Bodi ya Benki hiyo hivi karibuni.
Mkurugenzi huyo amempongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuwa kiongozi mwenye maono ambaye amesaidia katika mabadiliko makubwa ya uchumi na kuzitaka nchi nyingine barani Afrika kujifunza kutoka Tanzania.
“Nilipotua nimeona jengo la abiria la III katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, daraja la juu la Mfugale na ujenzi wa Reli ya Kisasa unaoendelea kwa kasi, miundombinu ambayo miaka miwili iliyopita sikuikuta nilipotembelea hapa nchini” alisema Bw. Cheptoo.
Aidha, amempongeza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kwa kusimamia na kuhakikisha uchumi unaendelea kuwa imara ikiwa ni moja ya lengo la Benki hiyo katika jitihada za kuifanya Afrika kuwa na uchumi imara.
Kwa upande Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amewataka watanzania kujivunia hatua za maendeleo zinazoonekana kwa kuwa hata wageni wanaona mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini.
Ameishukuru Benki ya AfDB kwa kukubali kufadhili miradi ya barabara za mzunguko Jijini Dodoma na pia miradi mbalimbali ya kilimo ambayo inaajiri watu wengi, huku akibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka minne miradi mbalimbali imetekelezwa kwa msaada wa AfDB na kuifanya Tanzania kukua kwa kasi kiuchumi.
Dkt. Mpango amewataka watendaji wa Wizara yake kuhakikisha wanawakutanisha viongozi wa Sekta Binafsi na Watendaji hao wa AfDB kabla ya kumaliza ziara yao nchini, ili kufanya mazungumzo yatakayosaidia kutumia fursa zilizopo katika Benki hiyo.
Aidha, Dkt. Mpango amewataka watanzania wenye vigezo kuchangamkia nafasi mbalimbali za kazi zinazotangazwa katika Benki hiyo ili kuongeza uwakilishi wa wananchi hasa kutoka Afrika Mashariki, ikizingatiwa nafasi zinazotangazwa ni za ushindani.
Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB imefadhili miradi 23 hapa nchini ikiwemo miradi 21 ya umma na miwili ya Sekta Binafsi, katika Nyanja za Nishati, miundombinu ya barabara, usafiri, kilimo, maji na usafi wa mazingira, yote kwa pamoja ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 2 nuta 1