Mkutano wa 19 wa taasisi za fedha nchini uliokuwa ufanyike jijini Arusha tarehe 21 na 22 Novemba 2019 sasa utafanyika Dar es Salaam kwa tarehe hizo hizo.
Mkutano huo ambao umeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) utawakutanisha washiriki wapatao 300 ili kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya ya sekta ya fedha nchini. Watakaohudhuria mkutano huo ni pamoja an mawaziri wakiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakuu wa taasisi za fedha, wachumi wabobezi, wanataaluma na washirika mbalimbali wa maendeleo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo na Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Kened Nyoni, alisema mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
Mada katika mkutano huo zitahusu ‘Matumizi ya teknolojia katika kukuza sekta ya fedha ili kuleta mapinduzi ya viwanda’; ‘Maeneo yenye fursa za uwekezaji katika sekta ya fedha’, ‘Vigezo vinavyochangia kujenga tabia za ukopaji’, ‘Jinsi ya kukinga vihatarishi katika sekta ya fedha’; ‘Namna ya kuoanisha sekta ya fedha na maendeleo ya viwanda’; na ‘Tathmini ya mchango wa sekta ya benki katika huduma jumuishi za kifedha nchini’.
Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikiandaa mikutano ya taasisi za fedha kila baada ya miaka miwili tangu miaka ya 1980. Katika mikutano hii, viongozi wakuu wa taasisi za fedha, yakiwemo mabenki, mashirika ya bima, mifuko ya hifadhi za jamii na taasisi zingine za fedha wamekuwa wakikutana na kujadili masuala mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla. Mkutano wa 18 wa taasisi za fedha ulifanyika mwaka 2016 jijini Arusha na mada kuu katika mkutano huo ilikuwa ni ‘Jinsi sekta ya fedha inavyoweza kuifanya Tanzania inufaike kiuchumi kutokana na uwepo wake kijiografia’ (Harnessing Tanzania’s Geographical Advantage: The role of financial sector).
Imetolewa na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki