Home Mchanganyiko CDEA WAFANYA MAJADILIANO YA JIJI BUNIFU KWA WAFANYABIASHARA WA SOKO LA MIKOCHENI...

CDEA WAFANYA MAJADILIANO YA JIJI BUNIFU KWA WAFANYABIASHARA WA SOKO LA MIKOCHENI B

0

Afisa mradi wa CDEA, Anjela Kilusungu akitoa mada katika mkutano wa majadiliano ya jiji bunifu (Creative City Dialogue).

Afisa mradi wa kampuni ya Zaidi Recyclers, Eva Msella akitoa juu ya faida ya taka kwa wakazi na wafanyabiashara wa soko la Mikocheni B

Baadhi ya wakazi na wafanyabiashara wa soko la Mikocheni B wakifuatilia mkutano huo wa majadiliano.

…………………………………………………..

TAASISI ya Utamaduni na Maendeleo Afrika Mashariki (CDEA) imeendesha majadiliano ya Jiji bunifu (Creative City Dialogue) kwa wakazi na wafanyabiashara wa soko la Mikocheni B, Jijini Dar es Salaam.

Katika majadiliano hayo CDEA kwa kushirikiana na taasisi ya Zaidi Recyclers kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswis wameweza kuwafikia wananchi hao wa Mikocheni B ambapo walijadili mada za urejelezaji (recycling) na fursa zake.

Awali akitambulisha mradi huo, Afisa mradi wa CDEA, Anjela Kilusungu alisema Urejelezaji (recycling) una fursa nyingi hivyo wananchi wachangamkie fursa hizo.

“CDEA kwa kushirikiana na wadau wetu tumeona ni vyema kutoa taarifa za urejelezaji ambapo kupitia njia ya majadiliano itasaidia kufikisha elimu na kupambanua kwa kina fursa zilizopo kama kipato, uhifadhi wa mazingira na kuboresha afya” alisema Bi Angela Kilusungu.

Angela Kilusungu aliwaomba wakazi wa Mikocheni wakiwemo wafanyabiashara wa soko hilo la Mikocheni B, waanze kutenga taka kama njia ya kwanza kabisa ya shughuli ya urejelezaji pamoja na kuwasihi kulitumia jalala lililopo katikati ya soko hilo kwa umakini ili liweze kuwa chanzo cha mapato katika soko hilo.

Kwa upande wake, Afisa Miradi wa Kampuni ya Zaidi recyclers Eva Msella aliweza kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao namna utenganishaji wa taka, uhifadhi na urejelezaji unavyokuwa fursa.

Eva Msella alisema kwa sasa taka zina faida endapo zitatenganishwa na kurejelezwa kuwa bidhaa mpya ambapo pia amewaelezea wananchi hao juu ya fursa ya taka ambazo zinaweza kuwaingizia kipato cha kuendesha maisha yao kwa kutengeneza taka hizo na kuwa bidhaa kama mbolea, mapambo na samani za majumbani.

Mjadara huo wa Jiji bunifu upo chini ya mradi wa “Taka Yangu, Hazina Yangu” ulioendeshwa kwa miezi sita katika kusaidia kupunguza tatizo la taka ngumu zinazodhalishwa jijini Dar es Salaam kwa tutumia sanaa chini ya usimamizi wa CDEA kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswis.