Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo wakati alipokuwa akizungumzanao ofisini kwake jijini Dar es salaam.
***************************
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo ameagiza kufukuzwa shule kwa mwanafunzi yeyote atakayebainika kuharibu kwa makusudi miundombinu au samani katika shule za umma kwa lengo la kuhakikisha usalama wa muda wote wa miundombinu hiyo.
Jafo ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumza na waandishi wa habari huku akiwataka wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za mitaa kuhakikisha shule zote katika maeneo yao zimeboresha fomu ya maelezo ya kujiunga na shule (Joining Instructions)
Alisema sababu ya kuboresha fomu hizo ni hatua inayolenga kuweka adhabu za kuchukuliwa dhidi ya mwanafunzi au kikundi cha wanafunzi kitakachobainika kufanya uharibifu huo.
Alisema hatua hiyo imetokana na tabia iliyoanza kujitokeza siku za hivi karibuni ikiwemo mkoani Mbeya na Morogoro kwa baadhi ya wanafunzi hao kufanya uharibu wa miundombinu na samani za shule, jambo alisisitiza kuwa ni kinyume na utaratibu lakini pia zikirudisha nyuma juhudi za Serikali na wadau wengine wa maendele katika suala la ujenzi wa shule hizo.
Alisema Serikali isingependa kuona uharibifu wa miundombinu hiyo ikitokea kama walivyofanya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mji Mpya ya Manispaa ya Morogoro na Shule ya Sekondari ya Kiwanja ya Halmashauri ya Chunya ambao wameonyesha nidhamu mbovu ya kuanza kuharibu miundombinu ya shule huku akiwapongeza viongozi katika mikoa hiyo kwa kuchukua hatua stahiki.
“Wazazi na walezi watawajibika kutengeneza kifaa au mali hiyo na kuirejesha katika hali yake ya awali, aidha mzazi au mlezi wa mwanafunzi atakayekiuka masharti hayo ya shule, mwanaye asimamishwe masomo au afukuzwe shule kwa maana hatuwezi kuvumilia kuendelea kuwa na wanafunzi waharibifu na wasio na maadili mema katika shule zetu” aliongeza Jafo.
Aidha alizitaka bodi za shule zifanye kazi yao ipasavyo ili kuilinda miundombinu hiyo na samani za shule na kuwaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha maendekeo ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na kusimamia nidhamu ya wanafunzi na watoto ambao ndiyo nguzo na viongozi wa baadae wa Taifa hili.