Aliyewahi kuwa mgombea wa Ubunge kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo katika Jimbo la Mkuranga Kunje Ngombale Mwiru akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuomba msajiri kuchukua hatua ya kuchunguza maamuzi ya vyama vya saisa vilivyojitoa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, Kulia ni Mwanaharakati Felix Makuwa anayeiwakilisha Taasisi ya Society Awareness.
Mwanaharakati Felix Makuwa anayeiwakilisha Taasisi ya Society Awareness akifafanua jambo katika mkutano huo, kulia ni Aliyewahi kuwa mgombea wa Ubunge kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo katika Jimbo la Mkuranga Kunje Ngombale Mwiru.
……………………………………………..
Wanaharakati wa masuala ya kisiasa aliyewahi kuwa mgombea wa Ubunge kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo katika Jimbo la Mkuranga Kunje Ngombale Mwiru pamoja na mwanaharakati mwenzie anayeiwakilisha Taasisi ya Society Awareness Felix Makuwa,wamemtaka Msajili wa vyama vya siasa kuvihoji vyama vilivyotangaza kujitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili aweze kubaini kama kweli maamuzi yao yalitokana na makubaliano ya halmashauri kuu za vyama hivyo lkama siyo ubinafsi wa viongozi wachache katika vyama hivyo.
Viongozi hao wamesema wanachoaamini wao viongozi wa ngazi za juu wa vyama hivyo wametoa maamuzi hayo bila maamuzi ya vikao halali ndani ya vyama hivyo wakidai kuwa mara nyingi viongozi hao wamekuwa wakurupukaji wanaofanya mambo yao kinyemela suala walilosema limekuwa likiua demokrasia ndani ya vyama hivyo.
Wamewataka watanzania kuachana na siasa ‘uchwara’ wanazodai kufanywa na vyama vilivyotangaza kujitoa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 Mwaka huu.
“Wanayoyasababisha haya yote yanayoendelea ni viongozi wa juu wa vyama vya upinzani, tena baadhi yao wameenda mbali na kukejeli kuwa vyama vingine katika uchaguzi huu havina hata wabunge bungeni hata vikiamua kushiriki, hiyo ni kejeli zaidi msajili anapaswa kuvifuatilia ili kuona kama vilijitoa kutokana na maamuzi ya halmashauri kuu za vyama hivyo” amesema Kunje.
Wamesema wanachoamini vyama hivyo vyenye wabunge ndiyo hasa vinavyoua suala la upinzani kwa kuwa mara nyingi wabunge wao hutoa ahadi hewa kwa wananchi kwa kuwatajia mambo mengi ambayo endapo watapewa ridhaa watawafanyia lakini mwisho wa siku huishia kuvimbisha matumbo yao bila kutekeleza jambo walilosema huwapa hasira wananchi hao na kukataa kuwapa kura zao kipindi kingine.
“Tena itapendeza kama msajili wa vyama vya siasa atawashughulikia wabunge hao ambao baadhi yao wamekuwa wakichukua posho za bure bungeni bila hata kuingia katika vikao vya bunge zaidi wamekuwa wakipiga kelele zisizo na tija na kusababisha maneno ya hovyo katika jamii”.Ameongeza Mwiru
Akitoa mfano Mwanaharakati Kunje Ngombale Mwiru amesema “Nilipotangaza kumuunga mkono Rais John Magufuli wakati Nikigombea Ubunge Mwaka 2015 katika jimbo la Mkuranga , niliona hakuna sababu ya kupoteza kura yake kumchagua rais asiye faa zaidi ya kiongozi huyo ambaye hadi sasa ameweza kuipa thamani kura yake kwa kufanya mambo mengi ya kimaendeleo nchini.
Ameongeza kuwa kama ingewezekana uchaguzi ujao asisimame mgombea yoyote katika nafasi ya kiti cha urais na kumuacha Rais Magufuli aendelee na nafasi yake ili kuokoa fedha ambazo zingetumika katika kampeni yake ziweze kwenda katika kuhudumia maendeleo.
“Rais aachwe katika nafasi yake, tukachague wabunge tu, anafanya mambo mazuri katika taifa hili ambayo kila mtanzania anayaona” Amesema Mwiru.
Naye Mwanahrakati Felix Makuwa amesema hii tabia ya kususasusa kutoka katika vyama vya upinzani siyo jambo la kushangaza kuona vikisusia tena uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa sababu ni mazoea yao na hii tabia inaua Demokrasia kwa sababu maamuzi ya kususia uchaguzi yanafanywa na vipongozi wa juu kwa kuwashurutisha wagombea wao ilihali wagombea bado wanataka kuendelea na uchaguzi .