Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Emmanuel Kakwezi (mbele) akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika Mkutano wa BRELA na vyombo mbalimbali vya Habari kuzungumzia mafanikio ya BRELA ndani ya Miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano. Mkutano huo umeandaliwa na Idara ya Habari Maelezo na umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar ea Salaam.
*************************************
Dar es Salaam,
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni
(BRELA) Bw. Emmanuel Kakwezi amesema kwamba, moja kati ya
mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya
awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Joseph Pombe Magufuli ni utoaji wa huduma zake zote kwa njia ya
mtandao.
Bw. Kakwezi ameyasema hayo akiwa katika mkutano na Waandishi wa
Habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC)
Dar es Salaam ulioandaliwa na Idara ya Habari Maelezo.
Ameeleza kwamba Wananchi wanaweza kuwasilisha maombi ya huduma
zote zinazotolewa na BRELA popote pale walipo nchini kwa Mfumo wa
Usaili kwa njia ya mtandao, (Online Registration System / ORS).
“Hivi sasa maombi yote ya Usajili yanatumwa kwa njia ya Mtandao, iwe ni
Usajili wa Kampuni, Usajili wa Jina la Biashara, usajili wa Alama ya
Biashara au Huduma, utoaji wa Leseni za Viwanda, utoaji wa Leseni za
Biashara kundi A na utoaji wa Hataza” amesema Bw. Kakwezi.
Bw. Kakwezi ameongeza kwamba Mabadiliko haya yanaambatana na faida
nyingi, ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa kufanya usajili, mathalani
usajili wa Kampuni hivi sasa unaweza kukamilika ndani ya siku moja.
Mfumo huu uwasaidia watumiaji kutuma maombi yao popote pale walipo
nchini nan je ya nchi vilevile.
Zaidi ya hilo mfumo huu unamsaidia mtumiaji kufuatilia maendeleo ya
maombi yake na kupata mrejesho kwa ajili ya kufanya marekebisho pale
maombi yanapoonekana kuwa na kasoro.
Aidha katika kipindi cha miaka minne, BRELA pia imefanikisha uanzishwaji
wa Shahada ya Uzamivu ya Miliki Ubunifu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Shirika la Miliki Ubunifu la Kanda (ARIPO) na
Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO).
Mpango huu una lengo la kuongeza elimu kwa Umma na wataalam katika
eneo la Miliki Ubunifu. Shahada hiyo ya Uzamivu imeanza kutolewa mwezi
Agosti 2019.
BRELA kwa kushirikiana na COSTECH pamoja na Shirika la Miliki Ubunifu
Duniani (WIPO) imetekeleza mradi wa Upatikanaji wa taarifa za teknolojia
zilizopo kwenye kanzidata za Hataza (TISCs) kwa ajili ya kutumiwa na
watafiti na watumiaji wengine ambapo jumla ya Hataza milioni sabini na
sita (76,000,000) zinaweza kupatikana kwenye kanzidata husika.
Katika kipindi cha Miaka minne, BRELA imefanikisha kuanzisha Utoaji wa
Leseni za Biashara kundi A na kundi B kwa njia ya mtandao. Mfumo huu
umeunganishwa na Mifumo ya Malipo ya Serikali yani Government
Electronic Payment Gateway (GEPG) na Mfumo wa Taarifa za Makusanyo
ya Mapato wa Mamlaka za Serikali za mitaa yaani Local Government
Revenue Collection Information System (LGRCIS).
Majaribio ya Mfumo huu yalianza tarehe 1 Oktoba 2019 na mpaka sasa
Leseni za Biashara Kundi A zinazotolewa na BRELA na Leseni za Biashara
kundi B katika Manispaa za Bukoba, Chalinze, Wilaya ya Karagwe,Mji wa
Mafinga, Manispaa za Ilala na Halmashauri za Jiji la Mwanza zinatolewa
kwa njia ya Mtandao.
Katika utoaji wa Leseni kwa mfumo huu takwimu zinaonesha jumla ya
Leseni za Biashara 1206 zimetolewa kupitia mfumo huo ambapo kati ya
hizo BRELA imetoa Leseni 470, Jiji la Mwanza Leseni 199 na Manispaa ya
Ilala Leseni 537.
Bw. Kakwezi ameeleza zaidi kwamba ndani ya miaka minne BRELA
imefanikiwa kuanzisha dirisha la Mfumo wa utoaji wa taarifa za Kibiashara
za Kimataifa. Dirisha hili linamuwezesha mtuamiaji au mwombaji kufahamu
taarifa mbalimbali za upatikanaji wa Leseni na vibali kwa bidhaa
zinazouzwa nje na zinazoingizwa ndani ya nchi.
Dirisha hili linatoa fursa kwa mwombaji kutembelea tovuti ya
www.trade.business.go.tz na kupata taarifa zote za Biashara zinazohusiana
na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi (Export) na uaigizaji ndani ya nchi
(Import).
Vilevile mtumiaji atafahamu Sheria, Kanuni, taratibu muda utakaotumika
pamoja na gharama za kila aina ya huduma (Administrative procedures)
atakayohitaji na wapi apite ili kufanikisha upatiakanaji wa huduma
anayohitaji.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ilianzishwa chini ya
sheria ya wakala wa serikali namba 30 ya Mwaka 1997 na hatimae
kuzinduliwa rasmi tarehe 3 mwezi Disemba 1999.
BRELA ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara na ilianzishwa kwa ajili
ya kuratibu shughuli za biashara na kudhibiti sheria pamoja na utoaji wa
huduma za Usajili wa Kampuni, usajili wa majina ya biashara, usajili wa
alama za biashara na huduma, utoaji wa leseni za viwanda, utoaji wa
leseni za biashara kundi, utoaji wa Hataza na Miliki bunifu.