Bi. Bettie Luwuge Afisa Mawasiliano kutoka shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG) akizungumza na wanakijiji wa Kijiji cha Diguzi Kata ya Matuli wilaya ya Marogoro mkoani Morogoro wakati waandishi wa habari walipotembelea mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’.
…………………………………………………
Uongozi na wanakijiji wa Kijiji cha Diguzi Kata ya Matuli wilaya ya Marogoro mkoani Morogoro wamesema Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’ umewaondoa kwenye utegemezi wa zaidi ya miaka 40.
Akizungumza leo Novemba 12,11,2019 na waandishi wa habari walitembelea kijiji hicho, Mtendaji wa Kijiji hicho, Redemter Matola amesema kwa hali ilivyo ni kwamba wanaelekea kusaidia vijiji vingine.
Matola amesema kabla ya mradi wa mkaa endelevu haujafika kijijini hapo kijiji hakikuwa na mapato ya aina yoyote ila mwaka mmoja wa utekelezaji wa mradi 2018/2019 kijiji kimefanikiwa kuingiza zaidi ya Sh.Mil 63.
“Maisha ya kabla ya mradi yalikuwa magumu kwani ofisi ya kijiji ilikuwa haina akiba yoyote hata kufikia kukosa fedha ya kununulia rimu kwa ujumla mkaa endelevu umetutoa kwenye utegemezi nadhani hali ikiwa hivi tutaanza kuwa wafadhili,” amesema.
Matola amesema mradi wa mkaa endelevu umeweza kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika sekta ya afya na elimu jambo ambalo halikutarajiwa huku uhifadhi ukiongezeka.
Mtendaji huyo amesema kutokana na mradi huo kuonesha matokeo chanya anaomba Serikali kuundeleza pale wafadhili watakapofikia kikomo kwani una tija kwa kijiji na nchi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi kupitia mradi wa mkaa endelevu Chilunda Iman, alisema maendeleo ambayo wamepata kwa mwaka mmoja wanadiriki kusema hawahitaji shilingi milioni 50 za ahadi ya Rais John Magufuli bali mradi uwe endelevu.
Alisema awali hawakujua kuwa wamekalia rasilimali muhimu huku wakiendelea kuwa maskini hivyo mradi huo umewafungua macho kwa kupata elimu, malengo na mipango ya kutumia fedha hizo.
“Sisi hatuhitaji Shilingi Milioni 50 za Rais kwa kila kijiji kwani tumeweza kutumia Shilingi Milioni 48 kati 63 zilizokusanywa. Tumejenga choo cha kijiji shilingi milioni 3, kuweka umeme jua kwenye Zahanati Shilingi Milioni 1, ukarabati wa tanki na Shilingi Milioni 1 na ujenzi wa nyumba ya mwalimu Shilingi Milioni 13.8.
Amesema pia zipo fedha zimetumika kwa ajili ya ulinzi wa msitu wa kijiji kwa kuwalipa posho walinzi na kugharamia fedha za vikao na shughuli nyingine za kijiji.
Iman amesema mradi huo umewezesha wananchi kutambua na kufuatilia mapato na matumizi ya kijiji jambo ambalo halikuwepo awali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji, Jonathan Biko alielezea changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa finyu kuhusu dhana hiyo.
Biko amesema changamoto nyingine ni vifaa duni vya ulinzi na wafugaji kuingiza mifugo kwenye misitu hali ambayo inaibua migogoro zaidi.
” Unaenda kukamata muhalifu kwa kutumia vyombo vya asili huku yeye ana silaha ya moto hii ni changamoto kubwa,”amesema.
Aidha, Biko amesema pamoja na changamoto hiyo wameendelea kulabiliana nazo kwa kufuata taratibu za kisheria.
Amesema katika msimu wa 2019/2020 wanatarajia kujusanya mapato zaidi ya Shilingi Milioni 60 ambazo zitatekeleza miradi mipya na kumalizia ya zamani.
Mweka Hazina wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji, Angelina Mugasa amesema mradi huo umeweza kuimarisha ndoa zao kwa kuwa mama na baba wanashiriki kutekeleza mradi.
“Ninachoona kwa sasa ni ndoa kuimarika kwani hakuna anayesumbua mwenzake bali tunashirikiana kuanzia ngazi ya familia, jamii na kijiji kwa ujumla,” amesema.
Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Bettie Luwuge amesema wameamua kushirikisha waandishi wa habari katika mradi ili waweze kujionea na kusikia kwa wanavijiii wanavyofaidika na rasilimali misitu ya vijiji.
“Sisi tuliona fursa hii ya misitu vijiji kama njia ya kuwawezesha wanavijiji na imeweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na kihifadhi,” amesema.
Ofisa Kujemgea Uwezo wa TFCG, Simon Lugazo amesema vijiji 30 ikiwemo Diguzi katika wilaya ya Morogoro, Kilosa na Mvomero vimeweza kunufaika kwa kujengewa uwezo wa kutumia rasilimali ya misitu kwa njia endelevu.
“Hiki ambacho mmesikia kwa wanavijiji ndio lengo letu sisi kama TFCH, Mjumita na TaTEDO kupitia TTCS chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC) kumtoa mwananchi wa kijijini kwenye umaskini,” amesema.
Jonathan Biko Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili kijiji cha Diguzi akisoma taarifa ya mapato na matumizi mbele ya waandishi wa habari na wanakijiji wa Kijiji wenzake wa kijiji cha Diguzi Kata ya Matuli wilaya ya Marogoro mkoani Morogoro wakati waandishi wa habari walipotembelea mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’.
Saimon Lugenzo akifafanua jambo wakati akizungumza na wanakijiji wa Kijiji cha Diguzi Kata ya Matuli wilaya ya Marogoro mkoani Morogoro wakati waandishi wa habari walipotembelea mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’.
Redempta Matola Afisa Mtendaji wa kijiji cha Diguzi Kata ya Matuli wilaya ya Marogoro mkoani Morogoroakijibu baadhi ya hoja wakati waandishi wa habari walipotembelea mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya kijiji wa Kijiji cha Diguzi Chilunda Imani Kata ya Matuli wilaya ya Marogoro mkoani Morogoro akitoa taarifa ya ujenzi na mipango ya ujenzi wakati waandishi wa habari walipotembelea mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’.
Jonathan Biko Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili kijiji cha Digiza akiwaonesha waandishi wa habari jinsi ya kuhifadhi misitu na kuvuna miti kwa ajili ya mkaa kwa njia ya Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’.
Jonathan Biko Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili kijiji cha Digiza akiwaonesha waandishi wa habari jinsi ya kukata miti kwa ajili ya mkaa na kuhifadhi misitu katika mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’.
Baadhi ya waandishi wa habari wakibadilishana mawazo wakati walipotembelea msitu wa Diguzi namna wanakijiji hao wanavyohifadhi msitu huo
Saimon Lugenzo akifafanua jambo wakatiakihijiwa na waandishi wa habari katika msitu huo.
Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Diguzi iliyojengwa kwa fedha za mradi huo.
Ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika shule ya msingi Lukose iliyopo katika kijiji cha Diguzi inayojengwa kwa mapato ya fedha za mradi huo.
Wanahabari wakitembelea vitalu vya mradhi huo.
Picha ya pamoja mara baada ya waandishi wa habari kutembelea mradi huo.