Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo akiwasikiliza mashuhuda wanaofahamu kuzurumiwa kwa nyumba ya Bi Sharifa Mbaruku mara baada ya kufika katika eneo hilo mapema leo asubuhi.
Muonekano wa nyumba aliyozurumiwa Bi Sharifa Mbaruku mkazi wa Magomeni mzimuni miaka mitatu iliyopita.
Bi Sharifa Mbaruku ,aliyezurumiwa nyumba yake akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurudishiwa nyumba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo mapema leo asubuhi
Baadhi ya wananchi waliofika katika eneo la nyumba ya Bi Sharifa Mbaruku aliyezurumiwa kwa kipindi cha miaka mitatu wakishuhudia akirudishiwa nyumba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo.
…………………….
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo amesimamia haki na hivyo kuwezesha kurudishwa kwa Nyumba ya mkazi wa Magomeni Mzimuni,Bi Sharifa Mbaruku aliyenyang’anywa kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.
Mhe. Chongolo alichukua maamuzi hayo leo alipofika kwenye nyumba ya Bi Sharifa ikiwa ni baada ya bibi huyo kupeleka malalamiko ya kudai kuzurumiwa na Bi Magrethi ambaye kwa sasa inadaiwa kuwa anaishi nje ya Nchi.
Akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya kufika katika nyumba hiyo ,Mhe. Chongolo amesema kuwa aliyemuondoa kwenye nyumba hiyo mwaka 2016 alifanya makosa na kwamba hakuwa na haki ya kumiliki nyumba hiyo.
Amefafanua kuwa kazi ya serikali ya awamu ya tano ni kutetea wanyonge wanaozurumiwa haki zao na kwamba akiwa Mkuu wa Wilaya hiyo amerudisha umiliki wa nyumba hiyo kwa mhusika ambaye ni Bi Sharifa.
Amesema “kuanzia hivi ninavyozungumza unarudi kwenye nyumba yako rasmi, wewe ndio mmiliki wa nyumba hii, kwahiyo nendeni mkaondoe mabati yote ambayo yamezungushiwa na sisi kama serikali tutawachukulia hatua wote waliohusika na mchezo huu.
Amefafanua kuwa kilichotendeka ni uonevu wa hali ya juu na kwamba serikali itamchukulia hatua kazi za kisheria kwani aliyemtoa alikuwa ameuziwa nyumba namba 159 kama ambavyo alikuwa ameuziwa mwenye namba 154.
“ Baada ya Magreth kuuziwa iwe ilikuwepo au haikuwepo, hakuwa na mamlaka ya kuja kuchukua ulichouziwa wewe, alitakiwa atafute alichouziwa yeye na hata kama angekikosa alipaswa kurudi kwa aliyemuuzia nasio kukufuata wewe, kwahiyo utaendelea kuishi kwenye nyumba yako kwa sababu ulifuata sheria na taratibu zote” amefafanua Mhe. Chongolo.
Katika hatua nyingine Mhe. Chongolo ametoa agizo na kuwataka wote wenye tabia ya kupora nyumba za watu hasa masikini na wanyonge kuacha mara moja kwani hatamuonea haya mtu yeyote aliyekuwa kwenye manispaa yake.
Kwaupande wake Bi Sharifa aliyezurumiwa nyumba hiyo, amesema kuwa Disemba 27 mwaka 2016 akiwa amelala ilikuja gari ya polisi wakiwa na diwani wa Kata ya Magomeni wakati huo Ally Kondo pamoja na Kuruthumu Ramadhani walimtolea vitu nje na kumtaka kuondoka katika nyumba hiyo bila kutoa maelezo yoyote.
Ameeleza kuwa hakujua sababu za yeye kuondolewa katika nyumba hiyo kwakuwa aliyemtoa alikuwa na nyumba yenye namba 159 Bolock X nakusema kuwa kilichofanyika ni uonevu na hivyo kumshukuru Mhe. Chongolo kwakuwasaidia masikini kurudishiwa haki zao.
“ Mhe. Mkuu wa Wilaya nakupongeza sana baba kwakutujali masikini, mungu akubariki na akupe maisha marefu , hata Mahakama pia inachangia kwakuwa awali ilikuja toleo la kwanza lilionyesha 159 Block four, toleo la pili 159 Block eigth, toleo la tatu halikuwa na namba ya nyumba kwakweli huu ni uonevu” amesisitiza Bi Sharifa.