Na.Mwaandishi Wetu,Chamwino
BARAZA la Madiwani Wilaya ya Chamwino, Mkoani Dodoma , limekataa kupokea na kujadili taarifa zote za kamati za kudumu za Halmashauri hiyo na kuagiza kuchukuliwa hatua za kisheria Mwandishi wa vikao (CC), Bernard Luhamu, wakimtuhumu kughushi saini za wenyeviti hao wa kamati.
Hii imefatia baada ya wenyeviti wote wa kamati za kudumu, ikiwemo ile ya Fedha, Uongozi na Mipango inayoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Samwel Kaweya, kushangazwa na hatua ya makablasha hayo kuonekana kusaini kwa saini zao, wakati hawakuwahi kusaini.
Hatua hiyo ilitokea juzi katika kikao cha Baraza la madiwani, kilichoketi kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji za kamati za kudumu kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Madiwani hao walimtuhumu mwandishi huyo wa vikao (CC) kuwa alidiriki kulidanganya Baraza kwa kughushi saini za Wenyeviti wa kamati hizo za kudumu, huku wakitilia mashaka baadhi ya vipengele vya taarifa iliyowasilishwa kikaoni hapo kunyofolewa.
Awali kabla ya Madiwani hao kufikia uamuzi huo wa kuikataa taarifa hiyo, Diwani wa kata ya Buigiri, Kenneth Yindi, aliomba muongozo, akihoji kutoonekana kwa baadhi ya taarifa.
Akijibu hoja ya muongozo huo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elias Kaweya, alikiri kutoonekana kwa baadhi ya vipengele vilivyojadiliwa kwenye kamati ya fedha.
“Mwenyekiti niwe mkweli juu ya hili, mimi kama mjumbe wa kamati ya fedha kuna mambo tuliyajadili kule na yalitakiwa kuwasilishwa kwenye kikao hiki cha baraza lakini havionekani”.
Kutokana maelezo hayo ndipo aliposimama Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Samweli Kaweya na kukiri kuwepo kwa tatizo hilo la baadhi ya taarifa kunyofolewa, huku akishangazwa na hatua ya taarifa hiyo kuonekana kusainiwa na yeye wakati hakuwahi kufanya hivyo.
“Mkurugenzi …hata hii saini inaonekana ni ya yangu, lakini niseme kweli mimi sijawahi kuja kusaini hili kablasha kama taratibu zinavyota na nashangazwa na hiki kilichotokea humu, labda wenzangu katika kamati wao walisaini” alisema Mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa Halmashauri alitumia nafasi hiyo kuwahoji Wenyeviti wa kamati za kudumu kama walihusika kusaini makablasha kama taratibu zinavyoagiza, ambapo kwa pamoja walikataa kuwa hawakuwahi kupitia na saini taarifa zilizowasilishwa.
Kutokana na mkanganyiko huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Athumani Masasi, alilazimika kumnyanyua Mwandishi wa vikao ili kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma za kughushi saini.
Akijibu tuhuma hizo mwandishi huyo wa vikao , licha ya kukiri kuwa utaaratibu huo umekuwa ukitumika mara nyingi kutokana na makubaliano kati yake na Wenyeviti hao.
Akifafanua zaidi mara baada ya kikao kumalizika, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Masasi alionekana kushangazwa na uamuzi wa madiwani kwani hata kama walibaini kuwepo kwa kasoro walipaswa kuwasiliana na ofisi yake mapema na kurekebisha.
“Kama mlivyomsikia CC …pale hakuna fojali bali kilichotokea ni Madiwani kutafuta sababu tuu, baada ya kutaka hoja ambazo hazikufuata taratibu ziingizwe kwenye ajenda za kikao” .
Mapema kulionekana dalili za kuvunjika kwa Baraza hilo kufuatia malumbano ya kikanuni kufuatia baadhi ya Madiwani kutaka baadhi ya hoja zilizoibuliwa kwenye kikao cha chama kuingizwa kama ajenda katika kikao hicho.
Baadhi ya taarifa hizo ambazo Madiwani walitaka ziingizwe kama ajenda kwenye kikao hicho ni azimio lao la kutaka taarifa ya fedha kiasi cha zaidi ya shiingi milioni 700 za maendeleo ya upimaji ardhi kupitia ufadhili wa LIC.
Nyingine ni taarifa ya baadhi ya watumishi wa Halmashauri kujigawia kwa upendeleo viwanja 19 bila kufuata taratibu , pamoja na gari la Halmashauri lililotolewa msaada na serikali ya Korea ya Kusini, kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikidaiwa kukodishwa kifisadi, huku dereva aliyekuta akiendesha gari hilo si mtumishi wa umma.
Taarifa nyingine ilimuhusisha mtumishi wa idara ya ardhi ndugu Joseph Towo kutumia watumishi na mitambo ya kampuni yake kuendelea kupima maeneo kinyemela bila ya kufuata taratibu na mitambo yake kukamatwa na diwani tarehe 13.10.19 na kukiri kosa mbele ya kikao cha kamati ya fendha,uongozi na mipango.