Mtafiti wa vifaa vya nyuklia wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania(TAEC), Christina Nyakyi akihakiki vifaa vya upimaji wa mionzi vinavyotumika kupimia mionzi isiyo ayonisha katika kaguzi maeneo mbali mbali zinazofanyika.
………………………………………………
Taasisi, Watafiti na makampuni mbali mbali hapa nchini yanayohusika na vyanzo vya mionzi isiyo ayonisha (Non Inonizing Radiation) kama vile makampuni ya simu (Base Tranasceiver stations),watumiaji wa vifaa tiba (MRI & Utra sound) wametakiwa kutembelea makao makuu ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) katika Kitengo cha Udhibiti wa Mionzi kwa lengo la kujifunza na kupata kupata ujuzi utakaosaidia kulinda usalama wa wafanyakazi, wananchi na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi isiyoayonisha.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtafiti wa vifaa vya Nyuklia, katika Idara ya Mionzi isiyo Ayonisha Injinia ,Christina Nyaki katika mahojiano maalumu ambapo amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia sana kuboresha ulinzi na usalama mahala pa kazi kwa wafanyakazi, wananchi na mazingira kuhusiana na mionzi ya aina hiyo hapa nchini.
“Tunatoa wito wa watafiti na makampuni kuja kupata ujuzi utakaowasaidia kujilinda ili kuwa salama katika maeneo yao ya kazi kwa lengo la kulinda binadamu na mazingira” alisema Nyaki.
Injinia Nyaki amesema kuwa Sheria namba 7 ya mwaka 2003 ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania(TAEC) inawapa mamlaka ya kusimamia na kukagua maeneo mbali mbali yenye mionzi isiyo ayonisha kama vile kwenye minara ya simu, vituo vya Usambazaji wa Masafa ya utangazaji, vituo vya rada, katika laini kubwa za usambazaji wa umeme na pamoja katika vifaa tiba .
Amesema pia Tanzania iko chini ya kamati ya Kimataifa ya Udhibiti wa Mionzi isiyo ayonisha ICNIRP (International committee for non-ionizing radiation) inawataka kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa watoa huduma za namna hiyo ili kujiridhisha wote wenye kutumia vifaa hivyo nchini kama wanakidhi vigezo husika.
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania(TAEC) ilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba 7 ya mwaka 2003 ambapo dhima yake kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya mionzi ili kulinda umma,wafanyakazi pamoja na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.