NA MWAMVUA MWINYI
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijiji cha Diguzi ,Kata ya Matuli Morogoro vijijini mkoa wa Morogoro, wameuangukia uongozi wa CCM wilaya,mkoa na hata Taifa kufuatili kura za maoni kijijini hapo, ambapo yupo mgombea aliyeshinda katika kura hizo kisha kukatwa kwa hali isiyoeleweka.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari, baadhi ya wakazi Maulid Lwambo, Ramadhani Makwangu, Amini Jonathani na Aisha Mohamed wamesikitishwa na hatua ya kukatwa jina la Nassoro Ramadhani ambae alishinda kwenye mchakato huo.
“Diwani Luca Lumomo anatusumbua sana, huyu ni jamii ya mfugaji, hivyo anataka kutumia nafasi yake kutaka kukiteka kijiji chetu kukifanya kiwe cha wafugaji, kwa kuwa yeye ni mfugaji hivyo anatumia nafasi hiyo kutaka Mwenyekiti wa kijiji chetu nae awe mfugaji,” alisema Lwambo.
Ameuomba uongozi wa juu wa CCM uangalie figisu hizo wanazofanyiwa huku wakidai diwani wao amekuwa tatizo kubwa kwa maendeleo ya kiniji chao.
Nae Ramadhani anayetetea kiti hicho alisema kuwa anafanyiwa figisu hizo ili mmoja wa wagombea anaetakiwa na baadhi ya viongozi apite.
Nae Lumomo alikanusha kujihusisha na figisu zinazotajwa, huku akisema kuwa kulikuwa na ongezeko la wana-CCM siku moja kabla ya kufanyika kwa kura za maoni, hatua iliyomlazimu mgombea wao nafasi hiyo kupinga.
Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Morogoro Anthony Mhando alieleza taarifa hizo anazisikia lakini hazijamfikia rasmi katika ofisi yake.
Alisema yeyote mwenye malalamiko afike ofisi za chama kukaa kiti kimoja kujua tatizo lilipo ili kuimarisha chama na kuendelea na uchaguzi kwa amani.