Home Mchanganyiko NMB YATOA MISAADA YA MILIONI 110 UKEREWE,TABORA,SONGEA

NMB YATOA MISAADA YA MILIONI 110 UKEREWE,TABORA,SONGEA

0

Cornel Magembe akipokea vitanda na mashuka kutoka kwa Meneja  wa NMB Kanda ya Ziwa – Abraham Augustino (aliyevaa suti), wakati wa hafla ya makabidhiano yaliyofanyika juzi wilayani Ukerewe. Benki hiyo imekabidhi msaada  wa vitanda  na mashuka kwa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, viti na meza za shule na chuo cha Murutunguru,vifaa vya ujenzi kwa Zahanati ya Bwasa na shule za msingi na Sekondari za wilaya ya Ukerewe vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 75. 

Sospeter Magese, Akikabidhi msaada wa Bati za Shule za Sekondari na Msingi kwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Erick Komanya. Benki ya NMB ilikabidhi viti na meza kwa shule za sekondari, vifaa vya unjenzi – bati 216, mbao na misumari kwaajili ya shule za msingi Kanyenye, Kalunde na Ikomwa vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 30.

Siriel Mchemba (Mwenye miwani) akipokea moja ya vifaa tiba kutoka kwa Meneja wa NMB Kanda ya Mashariki –  Baraka Ladislaus kwa ajili ya kituo cha afya Gairo mkoani Morogoro. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Agnes Mkandya na Mganga M.fawidhi wa kituo cha afya Gairo, Dk. Dastan Mshana.

Janeth Shango akikabidhi msaada wa bati 175 kwa Mkuu wa Wilaya ya Songea- Pololet Mgema kwa niaba ya shule ya Msingi Ndelenyuma katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea.

………………

NA MWANDISHI WETU

KATIKA kuunga juhudi za utatuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Afya na Elimu nchini, Benki ya NMB wiki iliyopita ilikabidhi misaada mbalimbali yenye thamani ya Shilingi Milioni 110 katika wilaya za Songea, Tabora na Ukerewe.

Thamani ya misaada hiyo ya vifaa vya ujenzi na vifaa tiba, vinaifanya Benki ya NMB kutumia zaidi ya Sh. Mil. 900 kununulia na kukabidhi vifaa hivyo kwa Shule za Msingi, Sekondari, Zahanati na Vituo vya Afya nchini kwa mwaka huu. – 2019

Wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, NMB imekabidhi misaada ya vifaa vya ujenzi, elimu na afya yenye thamani ya Sh. Mil. 75 kwa shule 14 za msingi na sekondari, Chuo cha Ualimu Marutunguru na Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe.

Msaada huo, ulitolewa na Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Augustino Abraham na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo (DC), Corneli Magembe, ambaye aliishukuru benki hiyo kwa uwezeshaji huo, alioutaja kama unaoenda kumaliza tatizo la uhaba wa vifaa kwa taasisi husika.

Mkoani Tabora, NMB imekabidhi viti na meza wenye thamani ya Sh. Mil. 30 kwa shule sita za Manispaa ya Tabora, tatu zikiwa ni za sekondari na nyingine tatu za msingi, msaada ambao ulipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Erick Komanya.

Hafla hiyo ilifanyika Sekondari ya Wavulana Tabora, ambako Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi, Sospeter Magese, alikabidhi mabati 216, mbao na misumari vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 15, kwa ajili ya Shule za Msingi Kanyenye, Kalunde na Ikomwa.

Aidha, NMB ikatoa msaada wa mabati 175 ya geji 28, yenye thamani ya Sh. Mil. 5, kwa ajili ya Shule ya Msingi Ndelenyuma, iliyopo katika Halmashauri ya Madaba, wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza kabla ya kukabidhi bati hizo katika hafla ambayo ilifanyika katika Shule ya Msingi Ndelenyuma, Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Janeth Shango, alisema kwa miaka kadhaa sasa NMB imekuwa mstari wa mbele kuchangia miradi ya mbalimbali ya  maendeleo.

“Mpaka ninavyoongea leo, kwa mwaka huu 2019 pekee, tayari NMB tumetoa misaada yenye thamani ya Shilingi Milioni 900, tumejikita zaidi kwenye miradi ya elimu, afya na majanga,” alisema Shango wakati wa hafla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika wilayani Songea.