Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony (mbele) akikagua chanzo cha maji cha mradi wa Longido katika Mto Simba uliopo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro ili kutazama uwezekano wa kutoa maji kwenye chanzo hicho na kupeleka Namanga.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony (katikati) akitoa maelekezo kwa wataalam kutoka Mamlaka ya Maji Arusha (AUWSA) wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa Longido. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony (kushoto) akitoa maelekezo kwa wataalam kutoka Mamlaka ya Maji Arusha (AUWSA) wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa Longido.
**************************************
Mamlaka ya Maji Arusha (AUWSA) imetakiwa kuharakisha zoezi la tathmini ya kupeleka huduma ya maji katika Mji wa Namanga ili kusaidia wananchi kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji.
Agizo hilo limetolewa na Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati wa ziara yake kwenye chanzo cha mradi wa maji wa Longido katika Mto Simba uliopo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro Novemba 4, 2019 kwa lengo la kujionea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wake.
Mhandisi Sanga alisema ameridhika na hatua aliyoishuhudia ya ujenzi wa mradi wa Longido hata hivyo aliitaka AUWSA kuhakikisha inatazama namna ya haraka ya kufikisha huduma ya maji kwenye mji wa Namanga kutoka kwenye chanzo cha mradi huo hasa ikizingatiwa kwamba mji huo unasumbuliwa na kero ya upatikanaji wa huduma ya maji.
“Ninawapongeza AUWSA kwa usimamizi mzuri wa mradi lakini nataka kuona mnafanya tathmini haraka ya namna ya kufikisha maji kwenye mji wa Namanga kwani kuna changamoto kubwa sana kwenye mji huo,” alisema Mhandisi Sanga.
Akizungumzia uwezekano wa kutumia chanzo hicho cha Mto Simba kupelekea maji Namanga, Mhandisi Sanga alisema maji yaliyopo yanaonekana kuwa mengi na yanaweza kutosheleza kuhudumia maeneo yote mawili sambamba na maeneo mengine ya jirani.
“Tumekuja hapa kuona uwezekano wa kutoa maji kwenye eneo hili ili kufikisha Namanga, na nilichoshuhudia ni kwamba chanzo hiki kinaonekana kuwa na maji ya kutosha kwa maeneo yote mawili yani Longido na Namanga,” alisema.
Aliwataka kufanya mawasiliano ya haraka na Bonde la Pangani ili kuharakisha zoezi la tathmini ya kuona kiasi cha maji kinachoweza kuongezwa ili kuwezesha kupeleka maji kwenye mji wa Namanga kutoka kwenye chanzo hicho bila kuathiri matumizi ya asili ya chanzo hicho.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba alisema mradi wa Lingido umelenga kuongeza upatikanaji wa maji katika mji mdogo wa Longido kutoka asilimia 15 za sasa ambazo ni sawa na wananchi 2,510 hadi kufikia asilimia mia moja ambayo ni sawa na wananchi 16, 712.
Mhandisi Rujomba aliongeza kuwa malengo hayo ni hadi kufikia mwaka 2025 na kwamba hadi kukamilika kwake utakuwa umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 15.8. Aidha aliongeza kuwa wamepokea maagizo ya Naibu Katibu Mkuu na wanaanza kufanyia kazi maramoja.
Mhandisi Sanga yupo Mkoani Arusha akiendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji inayotekelezwa mkoani humo kwa lengo la kujionea hali halisi ya utekelezaji sambamba na kuelewa changamoto zilizopo ili kuzipatia ufumbuzi wa haraka.