Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI), Mh. Suleiman Jaffo (kulia), Mkurugenzi wa M-Pesa (katikati) Epimack Mbeteni pamoja na Mkurugenzi wa Vodacom Business, Arjun Dhillon (kushoto) wakizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa Ushirikiano baina ya
TAMISEMI na Vodacom ambao utawezesha Ofisi 127 za serikali za mitaa kupokea malipo kupitia M-Pesa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI), Mh. Suleiman Jaffo (kulia), Mkurugenzi wa M-Pesa Epimack Mbeteni (katikati) pamoja na Mkurugenzi wa Vodacom Business, Arjun Dhillon (kushoto) wakizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa Ushirikiano baina ya
TAMISEMI na Vodacom ambapo zaidi ya wateja milioni 14 watanufaika na matumizi ya M-Pesa katika malipo ya halmashauri na manispaa kote nchini.
************************************
Wateja zaidi ya milioni 14 wa Vodacom watanufaika na
huduma ya malipo kwa M-Pesa kwenda halmashauri na
manispaa mbali mbali nchini. Kampuni ya Vodacom
Tanzania kwa kushirikiana na ofisi ya TAMISEMI
wamefanikisha kuimarisha mfumo wa malipo ya kifedha
kwa kusogeza huduma ya malipo kwa M-Pesa kwa ofisi
zaidi ya ofisi 127 za serikali za mitaa nchini.
Uzinduzi wa huduma hiyo, ulifanyika ofisi za Makao Makuu ya
Vodacom, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa
(TAMISEMI), Mheshimiwa. Suleiman Jafo,
Akizungumza katika hafla hiyo, Mh Jafo alisitiza
umuhimu wa kutumia njia za kidigitali kama M-pesa
kufanya malipo na kukusanya mapato kwani itaboresha
uwekaji wa kumbukumbu, utoaji wa taarifa, kupunguza
uvujaji na ubadhirifu pamoja na kuongeza mapato kwa
idara mbali mbali za Serikali ndogo.
“Malipo kutumia njia hizi za kidigitali yanapunguza muda
mwingi tuliokuwa tunatumia kupanga foleni kufanya
malipo. Sasa tuna M-Pesa naamini muda huu
tutaupeleka moja kwa moja kwenye kujenga taifa na
shughuli za maendeleo. Napenda kuwapongeza
Vodacom kwa kutukumbuka na sisi huku TAMISEMI.
Ninatumaini kwamba huduma hii itawarahisishia malipo,
si tu kwa wananchi bali hata nyinyi viongozi katika
kutunza hesabu zenu,usalama wa fedha pamoja na
ukusanyaji fedha kwa ujumla,” aliongeza Jafo.
Kwa upande wake, Mkurugenziwa huduma ya M-Pesa,
Bwana Epimack Mbeteni alisema kupitia M-Pesa,
Vodacom inategemea kufikia taasisi nyingi za serikali na
binafsi ili kuwezesha mfumo wa malipo kuwa
rahisi,fanisi na salama zaidi.
“Asilimia kubwa ya watanzania wanatumia M-Pesa kufanya miamala mbali
mbali kama Luku, bili za maji, faini za barabarani, ndio
maana tukaona fursa kubwa ya kurahisisha malipo kwa
serikali za mitaa kutumia M-Pesa,” aliongeza Mbeteni.
Ushirikiano huu baina ya TAMISEMI na M-Pesa
utawawezesha wateja wa mtandao wa Vodacom
kufanya zaidi ya malipo 205 ya serikali za mitaa kwa
urahisi na usalama zaidi zaidi.Malipo kama vile leseni za
biashara, vibali vya ujenzi, malipo ya maegesho na
nyinginezo.
“Wote tunashuhudia jinsi M-Pesa inavoendelea
kubadilisha mfumo wa malipo nchini, ni tegemeo letu
kwamba, malipo katika serikali za mitaa hizi yatakuwa
rahisi na salama zadi.
Ili kulipa kupitia M-Pesa anaingia kwenye menu yake ya
M-Pesa *150*00# anachagua lipia bili, alafu malipo kwa
serikali za mitaa kisha anaweka namba ya kumbukumbu
ambayo atapatiwa na ofisi za serikali za mtaa au
anaweza kutumia APP ya M-Pesa kufanya malipo
wakati wowote,” alifafanua Mbeteni.