Home Mchanganyiko KIVUKO CHA KUBEBA ABIRIA NYAMISATI-MAFIA KUKAMILIKA NA KUANZA KAZI FEB 2020

KIVUKO CHA KUBEBA ABIRIA NYAMISATI-MAFIA KUKAMILIKA NA KUANZA KAZI FEB 2020

0

KIVUKO cha kubeba abiria kutoka Nyamisati, wilaya ya Kibiti ,kwenda kwenye Kisiwa cha Mafia mkoani Pwani ambacho ujenzi wake utagharimu sh.bilioni 5.3 kinatarajiwa kukamilika Februari 2020 .
Kukamilika kwa ujenzi huo itakuwa mkombozi kwa wasafiri wanaokwenda na kutoka kisiwani humo.
Hayo yalibainishwa na kaimu mkurugenzi huduma za vivuko ,Mhandisi Adelard Kweka wakati akitoa maelezo kwa kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani ,walipotembelea kuangalia ujenzi wa kivuko hicho unaofanywa na kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd ya Mwanza.
Alieleza, ujenzi wa kivuko hicho tayari umeanza na unatarajia kufanyika kwa kipindi cha wiki 40 , kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100 sawa na abiria 200 na magari madogo sita pamoja na mizigo.
Kweka alisema, kwa kupitia wakala wa ufundi na umeme (TEMESA) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 serikali imepanga kununua vivuko vipya vinne kwa ajili ya maeneo ikiwemo  Mafia-Nyamisati,Kayenze-Bezi,Bugolora-Ukara na Chato-Mkome na kufanya wawe na uwezo wa kuhudumia vivuko 34.
“Tunatarajia kitakamilika kwa muda uliopangwa kwani mkandarasi kalipwa kulingana na mahitaji na kinachosubiriwa ni kukamilisha kazi kwani hakuna tatizo lolote la kifedha kwa ajili ya kivuko hicho cha kisasa,” alisema Kweka.

Nae mkandarasi wa kivuko hicho, Saleh Songoro alibainisha, baadhi ya vifaa tayari vilishaingia na wanaendelea na ujenzi na baadhi ya vifaa vingine vitawasili mwezi wa 12 mwaka huu ikiwa ni pamoja na injini.
Songoro alisema hadi mwezi wa pili mwishoni kivuko hicho kitakuwa kimekamilika na kuanza majaribio kutoka Dar es Salaam kwenda Nyamisati na kufanya makabidhiano na safari zake.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno alisema, ujenzi wa kivuko hicho itakuwa ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Nyamisati na Mafia kwani itarahisisha usafiri ambapo kwa sasa usafiri mzuri ni wa ndege pekee.
Maneno alisema kuwa Rais Dk John Magufuli ameweza kujibu changamoto ya usafiri wa Nyamisati Mafia kwani ilikuwa ni kama donda ndugu ambalo lilikosa tiba lakini sasa limepata tiba.
Wakati huo huo msimamizi wa gati ya Nyamisati ambaye pia ni meneja wa bandari ya Dar es Salaam mhandisi Elihuruma Lema alisema kuwa gati hiyo imeshakamilika kinachosubiriwa ni makabadhiano.
Alifafanua, usanifu na ujenzi ulifanywa na kampuni mbili za  Alpha Logistics Tanzania Ltd na Southern Engineering Company Ltd ambazo zimekamilisha kazi hiyo ambapo gharama zilizotarajiwa ni kiasi cha sh.bilioni 14 japo zilipunguwa kutokana na ustadi wa ujenzi uliokuwa wa mwaka mmoja.