Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe Stella Ikupa,akisalimiana na Diwani wa Kata ya Buigiri Mhe. Kenneth Yindi alipowasili kwa ajili ya kufungua mafunzo ya Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu katika Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma
Mkurugenzi wa NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama,akitoa taarifa wa ufunguzi wa mafunzo ya Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu katika Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma
Diwani wa Kata ya Buigiri Mhe. Kenneth Yindi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu katika Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe Stella Ikupa,akizungumza na watu wenye ulemavu wakati akifungua mafunzo ya Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu katika Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe Stella Ikupa,akiwatunuku vyetu baadhi ya wajasiriamali.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe Stella Ikupa,akikata utepe kuashiria ufunguzi wa mafunzo ya Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu katika Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma.
…………………………….
Na.Alex Sonna,Chamwino
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe Stella Ikupa,amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika kutoa elimu kwa watu wenye uhitaji maalum ili kuweza kuwanasua katika kundi la ombaomba na kuwafanya wawe tegemezi kwa kuwa na miradi yenye kuwapa kipato.
Kauli hiyo ametoa wakati akifunga mafunzo ya Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu katika Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma.
Mafunzo hayo yalianza toka Novemba 29 ambapo yaliandaliwa na Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU kwa kushirikiana na Diwani wa Kata hiyo Mhe Kenneth Yindi ambapo yalihusisha watu wenye ulemavu na wanawake.
Elimu iliyotolewa ni Elimu ya kujitambua, Elimu ya usindikaji bidhaa kwa vitendo, Elimu ya masoko, Athari ya matumizi ya rushwa katika upatikanaji wa huduma, Umuhimu na utaratibu wa kuunda vikundi vya walemavu na wanawake pamoja na Elimu ya matumizi sahihi ya fedha za mikopo.
Mhe. Ikupa amempongeza Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama kwa uzalendo alionao kwa kuamua kutoa elimu kwa watanzania wenzake ambayo itawaondoa kwenye lindi la umaskini.
” Nikupongeze sana Jessica umefanya jambo kubwa siyo tu kwa Wananchi wa Buigiri bali kwa Taifa lako kwa ujumla. Elimu hii uliyowapa ina manufaa makubwa kwao wenyewe na hata kwa kizazi chao. Niwaahidi Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo katika kuwakomboa watu wetu,” Amesema Mhe Ikupa.
Amesema ili kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ni lazima kila kundi nchini lihusike katika uzalishaji na kuwapongeza wahitimu hao kwa kuelewa mafunzo vizuri na kuanza kutengeneza bidhaa zao ikiwemo Ubuyu, Siagi ya Karanga pamoja na Sabuni.
Awali Mkurugenzi wa NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa elimu ya kujitegemea watu wenye ulemavu ili kuepukana na dhana ya kwamba walemavu wote ni ombaomba.
Amesema Serikali ya awamu ya tano imepiga hatua kwenye maendeleo hivyo wao kama wadau wana kila sababu ya kusaidia Rais Magufuli katika kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
” Mhe Waziri tunashukuru kwa kufungua na kufunga mafunzo haya. Tunakuahidi kuwa Taasisi yetu itaendelea kutoa mafunzo haya Nchi nzima lakini pia kuwatafutia masoko ya bidhaa wanazotengeneza hawa wahitimu.
Tayari Dodoma tushatoa elimu kwa watu 300 hapa Chamwino na Wilaya ya Chemba, tutaenda Kongwa, Mpwapwa na Wilaya zingine. Lakini lengo letu ni kuona tunawainua kiuchumi walemavu na wanawake nchini,” Amesema Jessica.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Kenneth Yindi ameishukuru Serikali na Taasisi hiyo kwa kutoa mafunzo hayo ambayo anaamini yataenda kubadilisha mtazamo na fikra za wananchi wa Kata ya Buigiri.
Amesema mafunzo hayo yamewasaidia kuweza kujitambua na kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zitakua na nembo ya Buigiri jambo ambalo litasaidia Kata yao kukua kimaendeleo na kuvutia watu kuja kuwekeza na hivyo kuongeza mapato ndani ya Halmashauri yao.
” Hakika tunaipongeza Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU kwa kuendesha mafunzo haya, wametoa kiasi cha Sh Milioni Tatu za ueneshaji sambamba na walimu wawili, huu ni uzalendo mkubwa waliouonesha kwetu na tuwaombe waendelee kushirikiana na Serikali yetu ili kufikia kundi kubwa la watu wenye uhitaji,” Amesema Yindi.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, John Masaka ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa Maendeleo katika kufanikisha inawakomboa wananchi wake na kuahidi kutumia mafunzo hayo vizuri ili kujipatia kipato na kuepukana na dhana ya kwamba watu wa Dodoma ni ombaomba.
Pamoja na kuwakabidhi vyeti vya kuhitimu Naibu Waziri Ikupa alifungua pia Soko la Buigiri kwa ajili ya walemavu hao na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino kuwaongezea kiasi cha Sh Milioni Tatu ili waweze kukuza mitaji yao.