Home Michezo SIMBA SC YAMALIZIA HASIRA KWA MBEYA CITY,YAICHAPA  4-0

SIMBA SC YAMALIZIA HASIRA KWA MBEYA CITY,YAICHAPA  4-0

0

Na Asha Said, DAR ES SALAAM
MABINGWA watetezi, Simba SC wamezinduka na kupata ushindi wa 4-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
Simba SC inafikisha pointi 21 baada ya ushindi huo kufuatia kucheza mechi nane, ikishinda saba na kufungwa moja, wakati Mbeya City inabaki na pointi zake nane baada ya kucheza mechi tisa.
Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems ilipata bao lake la kwanza dakika ya nane kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa w Rwanda, Meddie Kagere aliyefunga kwa penalti baada ya Miraji Athumani ‘Madenge’ kuangushwa kwenye boksi.
Mzambia Clatous Chama akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 42 kwa shuti kali akiwa nje kidogo ya boksi baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Mbeya City inayofundishwa na kocha mzalendo, Juma Mwambusi kufuatia pasi ya kiungo mwenzake, Muzamil Yassin.
Simba SC ilipata pigo dakika ya 60 baada ya beki wake na Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Mbrazil Gerson Fraga ‘Viera.
Nyota wa Sudan, Sharaf Eldin Shiboub akaipatia Simba bao la tatu dakika ya 77 akimalizia pasi ya Ibrahim Ajibu, kabla ya kiungo mwenzao, Mkongo Deo Kanda kukamilisha shangwe za mabao za Wekundu wa Msimbazi kwa kufunga bao la nne dakika ya 86 akimalizia pasi ya Chama.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbao FC wamepata ushindi wa ugenini wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Coastal Union ilitangulia kwa bao la Shaaban Hamisi dakika ya 16 kabla ya Mbao FC kusawazisha kupitia kwa Waziri Junior dakika ya 64 na kupata la ushindi kupitia kwa Said Junior dakika ya 82.
Bao pekee la Adili Bahu dakika ya 77 likawapa ushindi wa ugenini Tanzania Prisons dhidi ya wenyeji, JKT Tanzania Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Na mabao ya Kassim Mdoe dakika ya 53 na Abdul Suleiman dakika ya 75 yaliipa ushindi wa 2-0 Ndanda FC dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Uwanja wa Ushirika mjini Moshi bao la kujifunga la Erick Mrilo dakika ya 59 liliipa ushindi wa 1-0 Polisi Tanzania dhidi ya Alliance FC ya Mwanza katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Gerson Fraga dk60, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Muzamil Yassin, Clatous Chama, Sharaf Shiboub, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/Deo Kanda dk79 na Miraji Athumani ‘Madenge’/ Francis Kahata dk46.
Mbeya City: Haroun Mandanda, Keneth Kinambi, Mpoki Mwakinyuki, Baraka Ngusa, Ally Lundenga, Samson Madeleke, Suleiman Mangoma, George Chota/Mohammed Mussa dk71, Peter Mapunda, Said Gamba na Richard Peter.