**********************************
NA MWAMVUA MWINYI, Chalinze
SHULE ya msingi Kibiki ,Chalinze mkoani Pwani ,ambayo ina wanafunzi 624 inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa matundu ya choo sita hali inayosababisha wanafunzi kutumia choo kimoja na walimu pamoja na upungufu wa madawati 150 .
Aidha shule hiyo ina mahitaji ya vyumba vya madarasa 14, yaliyopo matano upungufu tisa, hali inayowasababishia wanafunzi hao kusoma kwa mchanganyiko wa madarasa .
Kufuatia changamoto hizo, wadau mbalimbali na baadhi ya viongozi ukiwemo uongozi wa shule ya msingi ya Chalinze Islamic Modern kata ya Bwilingu ,umejitokeza kutoa msaada wa mifuko ya saruji 10 na maboksi ya karatasi nyeupe 15 kwa shule ya msingi Kibiki.
Hayo yalibainika wakati uongozi wa shule ya msingi Chalinze Morden ulipokwenda kujitolea nguvu kazi kwenye ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ya walimu, ambapo licha ya msaada huo pia wameshiriki katika nguvu kazi ya kuanza kwa ujenzi huo.
Akikabidhi msaada huo ,mkurugenzi wa Chalinze Modern ,Omary Swedy, alisema kuwa hatua hiyo wameifikia ili kuunga mkono juhudi za serikali kutatua changamoto zinayoikabili sekta ya elimu hapa nchini.
“Tulipata taarifa kuhusiana na shule hii ya Kibiki yenye zaidi ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwake, lakini inakabiliwa na changamoto lukuki, licha ya sisi kuwa na shule binafsi , tumeguswa na kuja kuwaunga mkono, sio kama sisi tunacho sana,ila kutoa ni moyo” alisema Swedy.
Swedy aliwaomba ,wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt.John Magufuli, kwa juhudi anazozionyesha kupambana na wabadhilifu wa mali ya umma, kuinua na kuboresha maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na kukuza kwa kasi uchumi wa nchi.
Nae mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kibiki, Magreth Kileo alishukuru kwa kupata msaada huo, na kusema wana mahitaji ya vyumba vya madarasa 14 ,yaliyopo matano upungufu tisa,madawati yapo 70 ,mahitaji 250 na pungufu ni 130 hali inayosababisha baadhi yao kukaa chini na kupelekea kuchafuka ovyo.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Bwilingu Lucas Rufunga ,alieleza kwa sasa ,wameanza kwa kujitolea nguvu kazi kuchimba msingi wa ujenzi wa madarasa matatu ,wazazi kuchangia matofali mawili .