Afisa anayeshughulikia Masuala ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dorice Mhimbila akizungumza na watu wasiosikia wa mkoa wa Simiyu wakati mamlaka hiyo ilipokwenda kutoa elimu ya utumiaji wa mawasiliano.
Baadhi watu wasiosikia (viziwi) wakiwa katika mafunzo ya utumiaji wa mawasiliano .
*********************************
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa imeendesha semina ya siku moja kwa watu wenye matatizo ya kutosikia (Viziwi) katika Mkoa wa Simiyu yenye lengo la kuwajengea uelewa juu ya matumizi sahihi na salama ya mawasiliano.
Mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambapo zaidi ya viziwi 50 wameshirikia mafunzo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa TCRA , Mhandisi Francis Mihayo amesema kuwa TCRA imeandaa mafunzo hayo kwa viziwi ili waweze kuepuka na madhara ambayo wanaweza kupata ikiwa watatumia vibaya mawasiliano.
Mihayo ameongeza kuwa viziwi ni moja kati ya watu ambao wameendelea kukumbwa na tatizo la matumizi mabaya ya mitandao kama facebook, instagram, whatsap na twitter kwa kurusha vitu ambavyo siyo sahihi.
“ Mara nyingi wamekuwa wakijikuta wakichukuliwa hatua kali za kisheria kwa kikuka sheria zilizopo za matumizi sahihi ya mawasiliano, kutokana na hali tumeona ni vyema tukawapa elimu jinsi gani ya wanaweza kuepuka kwa kuzitambua sheria,” amesema Mhandisi Mihayo.
Aidha Mihayo amesema kuwa amekuwa wakipata malalamiko mengi kutoka kwa viziwi juu ya kutapeliwa kupitia simu, ambapo kupitia mafunzo hayo wataweza kuwafundisha namna bora ya kuepuka hali hiyo.
“ Tunawaelimisha pia umuhimu wa kusajili laini zao kwa njia ya alama za vidole, tunatambua changamoto wanazozipata katika zoezi hili, ndiyo maana tumewaita hapa ili kuwapatia elimu na kutatua changamoto hiyo,” alisema Mihayo.
Akiongea kwa niaba ya viziwi hao Makamu mwenyekiti wa viziwi mkoa, Alex Benson viziwi wameeleza kukumbwa na tatizo la mawasiliano baina yao na watu wanaohusika katika zoezi la kusajili laini za simu kwa njia ya alama za vidole (Biometric Registration).
Wamesema kuwa tatizo hilo limesababisha viziwi wengi katika mkoa huo kushindwa kujisajili, kutokana na kushindwa kuelewana na watoa huduma wa makampuni mbalimbali ya simu wakati wa kujisajili kwa mfumo huo.
Bensoni alisema kuwa mbali na tatizo hilo, Bado Viziwi wameendelea kukumbwa na tatizo la kutapeliwa na watu wenye nia mbaya kupitia simu, ambapo alisema kupitia mafunzo hayo wataweza kutatuliwa changamoto hizo.
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga ameipongeza TCRA kwa kuona umuhimu wa zoezi hilo, kwani viziwi wanayo haki ya kupata elimu ya mawasiliano kama watu wengine.