*****************************
Dkt. Bashiru Ally Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Asubuhi ya leo, ametembelewa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar es salaam.
Viongozi hao wa Baraza la Wawakilishi pamoja na mambo mengine, wamempongeza Katibu Mkuu kwa kuendelea kufanya kazi ya kukiimarisha Chama na hasa kusimamia misingi ya haki na usawa katika kipindi hiki cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara, ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba, Mwaka huu.
Aidha, akizungumza na viongozi hao, Dkt. Bashiru amewahakikishia kuwa, CCM imejipanga kuhakikisha inashinda kwa kishindo na ushindi wa awamu hii utakuwa ni ushindi wa kihistoria katika Chama Chetu.
“Hakuna wa kuizuia CCM kushinda kwa kishindo awamu hii, Chama kimetimiza wajibu wake na wananchi wanaona mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana kupitia serikali ya awamu ya tano, hivyo ushindi wa kishindo ni hakika.” Dkt. Bashiru
Wajumbe hao kutoka Baraza la Wawakilishi ni Ndg. Rashid Shamsi Jimbo la Magomeni Zanzibar, Shaibu Ali Said (Chonga), Mtumwa Yusuph (Bumbwini), Masoud Masoud (Bububu), Bihindi Khamis Mkoa wa Kaskazini Pemba (viti maalum).