Home Mchanganyiko Rais Magufuli Angoa Mizizi ya Kufanya Kazi kwa Mazoea

Rais Magufuli Angoa Mizizi ya Kufanya Kazi kwa Mazoea

0

Na Lillian Shirima–Maelezo

Imetimia miezi 48 sasa sawa na miaka minne tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipochukua jukumu rasmi la kuiongoza nchi Novemba 5, 2015.

Kiongozi huyu amefanikiwa kuhakikisha watanzania wanatoka hatua moja kwenda nyingine kimaendeleo badala ya kubaki kama walivyo miaka nenda miaka rudi. Aina ya uongozi wa rais Magufuli umeonesha uwezo au karama ya kuondoa taratibu zilizooleka katika jamii na kisha kubuni, kuelekeza njia sahihi kwa vitendo ni ushindi wa mafanikio katika uongozi wake.

Katika kipindi kifupi rais Magufuli  amekuwa gumzo ndani na nje ya nchi kutokana  na uwezo alionao kushawishi watu kufikia maendeleo yaliyotarajiwa kwa kuondoa taratibu zisizofaa  kama vile uzembe kazini, ubadhirifu wa mali ya umma, na huduma mbovu za jamii kama vile maji safi na salama, elimu, afya.

 Akihojiwa na Idara ya Habari Maelezo mchambuzi  na mtafiti wa wa masuala ya uchumi na siasa Dkt.  Bravious Kahyoza anamuelezea Rais John Pombe Magufuli kama kiongozi  mwenye uthubutu wa kuamua mambo mazito na kuyatekeleza kwa wakati kwani   ameweza kuvunja taratibu zisizofaa ambazo zilikuwa kizingiti cha maendeleo ya nchi jambo ambalo limemjengea imani kwa wananchi .

“hakuna jinsi nyingine kubwa ya kuhakikisha watu wanatoka hatua moja kwenda hatua nyingine kama taratibu za maisha yao zinabaki zilivyo na tafsiri za kiuchumi duniani zinaonesha kuwa maendeleo ya watu kiuchumi  yanahusiana na utaratibu wa maisha ya watu wenyewe, Rais wetu amevunja taratibu korofi ”. Anasema Dkt. Kahyoza.

Aidha, ameongeza kuwa kinachomtofautisha rais Magufuli na viongozi wengine kiasi cha kusababisha awe gumzo ndani na nje ya nchi ni muda mfupi aliotumia kuleta mageuzi makubwa nchini.  Pia namna alivyoonesha mfano wa kubana matumizi katika kutekeleza majukumu yake kama kiongozi wa nchi. 

Mwandishi David Lender katika kitabu chake cha ‘The Wealth and Poverty of Nations: why some are so rich and some are so poor (Utajiri na Umasikini wa Mataifa: kwanini mengine ni tajiri na mengine masikini.  Kitabu hicho kimeeleza kwamba mataifa ambayo yameweza kuwa na sehemu kubwa ya mabadiliko kati ya miaka 1961 na 2014 ni yale  yaliyobadilisha taratibu na tabia za watu zilizooeleka na kuzielekeza kwenda kwenye mtazamo wenye tija kwa taifa lao, miongoni mwa mataifa hayo ni ulaya na Asia katika nchi za Uingereza, Japan na Afrika ni nchi za Namibia, Botswana, Rwanda na Ethiopia.

Anasema, mfano hai ni kama vile uandaaji wa sherehe za kitaifa za gharama kubwa, sherehe  wakati wa uteuzi wa viongozi mbalimbali, kumbukumbu za kitaifa, sherehe za uhuru, muungano na uzinduzi wa miradi ambapo fedha nyingi hutumika kusherehesha wakubwa serikalini na baadhi ya jamii.

Rais Magufuli  alichukua hatua ya kubatilisha taratibu za ufanyaji wa sherehe hizo kwa kufanya kazi za kijamii kama vile usafi, kuhudumia wagonjwa na mara kadhaa kutumia fedha husika kwa ajili ya manufaa ya taifa ambapo sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya uhuru aliagiza fedha zitumike kwenye ujenzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco. 

Pia, Rais Magufuli alipounda Baraza  la Kwanza la Mawaziri 2015, Baraza lilikuwa mawaziri 19 tu huku baadhi ya wizara  zikibaki bila naibu mawaziri. Rais aligiza kiasi cha shilingi bilioni 2 zilizokuwa zitumike kwaajili ya semina elekezi kwa viongozi wapya zipelekwe Wizara ya Elimu kutunisha fungu la elimu bure ikiwa ni pamoja na kununua madawati ya wanafunzi.

Rais hakuishia hapo, alizuia safari za viongozi nje ya nchi  zisizokuwa za lazima na yeye mwenyewe kupunguza safari zake nyingi nje ya nchi na kuagiza balozi kumwakilisha katika masuala ya Kimataifa.

Aidha, uzoefu wake katika kulitumikia taifa kwa muda mrefu, aligundua ndani ya utumishi wa umma yapo makundi mawili ya wafanyakazi wanaolipwa mshahara kwa mazoea. Kundi la kwanza ni watumishi ambao kwenye kumbukumbu za utumishi wanaonekana waajiriwa  wa serikali wanaolipwa stahiki zote za utumishi lakini si watumishi ambao kwa idadi walikuwa 20,000.

Kundi la pili ni watumishi ambao kwa mazoea wanafanya kazi lakini hawana sifa kwa nafasi walizonazo kwa idadi walikuwa 14,000. Watumishi hao baadhi  walitumia vyeti visivyo sahihi kuajiriwa na wengine walifanya kazi za taaluma ambazo hawakuwa na ujuzi nazo.

Kwa mamlaka aliyonayo, Rais Magufuli alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha  watumishi wa aina hiyo wanaondolewa sehemu zao za kazi. Zaidi ya watumishi 10,000 walipoteza ajira na serikali iliokoa zaidi ya shilingi Bilioni 15 za mishahara hewa huku Wakuu wa Mikoa walioshindwa kutekeleza agizo hilo kwa usahihi nyadhifa zao zilitenguliwa.

Pengine hali hii ndio iliyokuwa inasababisha hasira dhidi ya serikali kwakuwa wananchi hawakuona huduma zinatolewa kama zinavyostahili. Dkt. Kayhoza alisema kuwa nanukuu maneno ya rais Magufuli “Naagiza wakuu wote wa mikoa hakikisheni watumishi hewa yaani ambao hawapo wanaondolewa kwenye orodha ya utumishi na sehemu zao za kazi’

Pia, matokeo yake ndani ya kipindi kifupi serikali iliweza kutangaza nafasi za kwa wenye sifa katika sekta nyingi mathalani  Tamisemi ilitangaza ajira mpya kwa walimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na sekta ya afya na nyingine nyingi. 

 Hii leo watanzania tunaona mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika utumishi wa umma.

Dkt. Kayhoza anasema, Rais Magufuli ameonyesha dhahiri kuwa kiongozi bora asiye mlalamishi bali ni kiongozi anayetafuta  ufumbuzi wa kila changamoto anayokutana nayo. Aidha, ni kiongozi mwenye uthubutu , maamuzi sahihi, mtekelezaji, mfuatiliaji wa maamuzi yake mpaka yanapokamilika. 

“Hii inaonesha dhahiri uwezo alionao wa kuzisoma nyakati na kuhakikisha nyakati hizi zinaweza kutafsiriwa si tu kwa nchi anayoiongoza lakini pia kuangalia uchumi wa nchi unategemea masuala gani yanatokea na namna gani yanaweza kusaidia nchi kwenda mbele”. Amesema Dkt Kahyoza.

Maamuzi mengine aliyoyafanya ni serikali yake kuhamia Dodoma. Hadi sasa Mawaziri wote chini ya Waziri Mkuu, Naibu Mawaziri, Makatibu  na Kurugenzi zote muhimu zimehamia Dodoma.

Uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma haukupewa kipaumbele kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita tangu ulipoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye 1970. Kutokana na umuhimu wa kuhamia Dodoma watumishi wa serikali waliokuwa makao makuu walihamia Dodoma.  Hili ni funzo kwetu ambapo tukiamua tunaweza kwani ndani ya matumizi na mazingira yetu ya kawaida inawezekana tukapanga na tukatekeleza mambo yetu wenyewe kwa ufanisi.

Akitoa mfano juu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kufua umeme katika Mto Rufiji Dkt. Kahyoza amesema “Licha ya mradi huu utakaozalisha kilowati 2115 za umeme kupingwa na kukabiliwa na vizingiti ndani na nje ya nchi, Rais Magufuli ameweza kuvunja vizingiti hivyo ambapo Julai mwaka huu alizindua rasmi ujenzi wa bwawa la mto Rufiji  utakaogharimu fedha za Tanzania za shilingi trilioni 6.5.  

Suala lingine ambalo rais Magufuli aliahidi kupambana nalo ni ukusanywaji wa kodi ambapo ukaguzi kwa kila sekta umekuwa mkubwa na matokeo yake ni kuongezeka kwa mapato ya taifa kutoka shilingi milioni mia nane kwa mwezi hadi kufikia shilingi trilioni 1.7 Septemba, 2019.

Rais alisema“unapouza toa risiti na unaponunua dai risiti”.  Alianza kwa kusisitiza kwa mtu mmoja mmoja kudai risiti kwa kila huduma anayopatiwa  na baadaye akahimiza wafanyabiashara kulipa kodi ikiwa ni pamoja na taasisi za serikali kulipa kodi baada ya kupatiwa huduma  au bidhaa.

Hali hii imeleta mageuzi kwa kila mfanya biashara kuwa na mashine ya EFD (Eletronic Fiscal Divice) kitu ambacho hakijawahi kutokea miaka iliyopita. Amemalizia Dkt. Kayhoza

Naye Projestus Rwegarulila Mkurugenzi wa Mradi wa Utamaduni na Uzalendo anasema, Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kutumia lugha ya Kiswahili kwenye mikutano mbalimbali ya Kimataifa anayoshiriki  jambo halijawahi kufanyika kwa viongozi wetu hivi karibuni. 

 “Kitendo cha Rais kuongea Kiswahili kwenye mikutano ya kimataifa kimewalazimu wasiojua lugha hiyo kutafsiriwa na wengine kuamua kujifunza Kiswahili”. Anasema Rwegarulila.

Anasema, pamoja na watu kuvutiwa na kile anachozungumza Rais kwenye mikutano, kasi ya maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali ndiyo inawavuti wageni kuja kujifunza namna ambavyo nchi imepiga hatua  kama vile mradi kama vile mwendo kasi, kuanzishwa kwa sera sera mpya ya madini, ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme ni baadhi ya baadhi ya mambo yanayoamsha kiu ya mataifa mengine kujifunza kutoka kwetu.

Na hakuna lugha nyingine isipokuwa kutafsiri Kiswahili katika lugha zao.

Naye mwanafunzi Hamida Khamis wa shule ya msingi Bunge jijini Dar es Salaam amesema kabla ya serikali ya awamu ya tano shule yao haikuwa na madawati ya kutosha, wanafunzi walikuwa wanasukumana kutafuta nafasi za kukaa kwenye dawati lakini mpango wa elimu bure umefanikisha shule kupata madawati ya kutosha. 

Mkazi wa Mugumu Serengeti Herman Peter yeye anasema, kabla Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani huduma za afya zilipatikana katika Halmashauri ya Serengeti tu lakini sasa huduma zimesogezwa karibu baada Serikali kujenga Kituo cha Afya katika kata yao ya Nata kwa gharama ya shilingi milioni 400. 

Nimalizie kwa kusema  vema tukafahamu Rais John Pombe Magufuli ameweza kuondoa taratibu  zilizokuwa zikichelewesha nchi kusonga mbele. Hakuleta sheria mpya au sera mpya, alichokifanya ni kuhakikisha yeyote anayepewa dhamana ya uongozi anatimize  wajibu wake, anaposhindwa kuleta mabadiliko ndani ya muda mfupi anamwondoa katika madaraka aliyokuwa nayo. 

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.