Home Mchanganyiko Mwalimu Anaetuhumiwa kumvunja Mgongo Mwanafunzi Afikishwa Mahakamani Njombe

Mwalimu Anaetuhumiwa kumvunja Mgongo Mwanafunzi Afikishwa Mahakamani Njombe

0

**************************************

 JOCTAN MYEFU KUTOKA NJOMBE

Mwalimu Focus Mbilinyi anayetuhumiwa kwa  kumuadhibu mwanafunzi  wa darasa la tatu  kwa viboko  huku  akiwa amemning’iniza dirishani  na baadaye mwanafunzi huyo kuangukia mgongo  na kuvunjika uti wa mgongo amefikishwa  katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe  kwa ajili ya  kujibu  kosa la kuadhibu na kujeruhi.

Kesi namba 141 ya mwaka 2019 ya jamhuri dhidi ya Focus Mbilinyi iliyosomwa na mwendesha mashtaka Elizabeth Mallya mbele ya hakimu mkazi Ivan Msaki  huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Octavian Mbugari pamoja naye Innocent Kibadu

Hakimu Ivan ameanza kwa kuwasikiliza mashahidi wawili wa upande wa  walalamikaji  ambao ni  mtoto  Hosea Manga anayedaiwa kuadhibiwa na kuumizwa na  mwalimu  huku shahidi wa pili akiwa ni baba yake mzazi  Boniface Manga.

Mtoto Hosea ameieleza mahakama kuwa mnamo tarehe 21 ya mwezi machi mwaka 2017  majira ya asubuhi  akiwa darasa la tatu katika shule ya msingi Madeke  mwalimu Focus Mbilinyi  alitoa zoezi la somo la hisabati likiwa na maswali 10 huku akitoa maelekezo kuwa  atakaye kosa ataadhibiwa kwa idadi ya maswali aliyokosa.

Hosea ameeleza kuwa ukafika wakati wa mwalimu kutimiza ahadi yake kwa wanafunzi walioshindwa kufanya vizuri huku yeye akiwa amekosa hesabu zote kumi ndipo ilipofika zamu yake akaambiwa atundike miguu juu  ya dirisha huku kichwa kikiwa chini na mwalimu kumwadhibu kwa viboko na baadaye hosea kuangukia mgongo .

Naye Boniface Manga ambaye ni baba mzazi wa mtoto  hosea ameieleza mahakama kuwa siku ya tukio alikwenda shuleni  kwa ajili ya kuonana na mtoto wake mwingine aliyekuwa anasoma shuleni hapo kwa ajili ya kumpatia maelekezo ya kifamilia ndipo alipokutana na walimu waliompasha habari za kuumia kwa Hosea.

Aidha Boniface manga ameeleza hatua alizochukua kumpatia matibabu mtoto Hosea kuanzia zahanati ya kijiji cha Madeke  ambako baadaye wakahamishiwa kituo cha afya cha Lupembe  na kisha kwenda hospitali ya kibena kabla ya kwenda hospitali ya Ikonda na baadaye hospitali ya rufaa ya muhimbili ambako walibainisha kuwa Hosea amevunjika uti wa mgongo.

Shauri hilo limeahirishwa mpaka tarehe 12 mwazi wa 11 mwaka huu  ambapo upande wa mshtakiwa  utatakiwa kutoa ushahidi.

Mtuhumiwa wa kesi hiyo ya kujeruhi yupo nje kwa dhamana.