**************************************
JOCTAN MYEFU KUTOKA NJOMBE
Mwalimu Focus Mbilinyi anayetuhumiwa kwa kumuadhibu mwanafunzi wa darasa la tatu kwa viboko huku akiwa amemning’iniza dirishani na baadaye mwanafunzi huyo kuangukia mgongo na kuvunjika uti wa mgongo amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe kwa ajili ya kujibu kosa la kuadhibu na kujeruhi.
Kesi namba 141 ya mwaka 2019 ya jamhuri dhidi ya Focus Mbilinyi iliyosomwa na mwendesha mashtaka Elizabeth Mallya mbele ya hakimu mkazi Ivan Msaki huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Octavian Mbugari pamoja naye Innocent Kibadu
Hakimu Ivan ameanza kwa kuwasikiliza mashahidi wawili wa upande wa walalamikaji ambao ni mtoto Hosea Manga anayedaiwa kuadhibiwa na kuumizwa na mwalimu huku shahidi wa pili akiwa ni baba yake mzazi Boniface Manga.
Mtoto Hosea ameieleza mahakama kuwa mnamo tarehe 21 ya mwezi machi mwaka 2017 majira ya asubuhi akiwa darasa la tatu katika shule ya msingi Madeke mwalimu Focus Mbilinyi alitoa zoezi la somo la hisabati likiwa na maswali 10 huku akitoa maelekezo kuwa atakaye kosa ataadhibiwa kwa idadi ya maswali aliyokosa.
Hosea ameeleza kuwa ukafika wakati wa mwalimu kutimiza ahadi yake kwa wanafunzi walioshindwa kufanya vizuri huku yeye akiwa amekosa hesabu zote kumi ndipo ilipofika zamu yake akaambiwa atundike miguu juu ya dirisha huku kichwa kikiwa chini na mwalimu kumwadhibu kwa viboko na baadaye hosea kuangukia mgongo .
Naye Boniface Manga ambaye ni baba mzazi wa mtoto hosea ameieleza mahakama kuwa siku ya tukio alikwenda shuleni kwa ajili ya kuonana na mtoto wake mwingine aliyekuwa anasoma shuleni hapo kwa ajili ya kumpatia maelekezo ya kifamilia ndipo alipokutana na walimu waliompasha habari za kuumia kwa Hosea.
Aidha Boniface manga ameeleza hatua alizochukua kumpatia matibabu mtoto Hosea kuanzia zahanati ya kijiji cha Madeke ambako baadaye wakahamishiwa kituo cha afya cha Lupembe na kisha kwenda hospitali ya kibena kabla ya kwenda hospitali ya Ikonda na baadaye hospitali ya rufaa ya muhimbili ambako walibainisha kuwa Hosea amevunjika uti wa mgongo.
Shauri hilo limeahirishwa mpaka tarehe 12 mwazi wa 11 mwaka huu ambapo upande wa mshtakiwa utatakiwa kutoa ushahidi.
Mtuhumiwa wa kesi hiyo ya kujeruhi yupo nje kwa dhamana.