Wanafunzi wa shule ya sekondari Measkron Wilayani Hanang’ wakiimba wimbo wakati wakimpokea Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alipotembelea shule hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizindua madarasa mawili ya shule ya sekondari Measkron Wilaya ya Hanang’.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti (kulia) akitoa maagizo kwa viongozi wa Wilaya ya Hanang’ alipotembelea shule ya sekondari Measkron.
******************************
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewapa muda wa miezi mitatu viongozi wa Kata ya Measkron Wilayani Hanang’ kuhakikisha wanamalizia ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari Measkron.
Mnyeti alitoa agizo hilo jana wakati alipotembelea eneo hilo na kufungua mradi wa madarasa mawili ya shule ya Measkron yaliyojengwa kwa sh35.9 milioni.
Alimtaka ofisa mtendaji wa kata ya Measkron, Mwajuma Kipengele kuhakikisha anasimama utekelezaji wa agizo hilo la umaliziaji wa ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara ya shule hiyo ya sekondari.
“Haiwezekani jengo la maabara ya kufundishia baiolojia, kemia na fizikia liwe halijamalizika hivyo mtendaji wa kata subiri upate viongozi wazuri wa serikali za mitaa watakaochaguliwa kisha muanze kazi,” alisema Mnyeti.
Hata hivyo, aliwataka wananchi wa kata hiyo kutumia fursa ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 24 mwaka huu kuchagua viongozi bora na wazuri.
“Wanafunzi wa sekondari ya Measkron wameimba ujumbe mzuri juu ya kushiriki uchaguzi ndiyo sababu nikawapa sh1 milioni ya chakula nanyi jipangeni msifanye makosa tena ya kuchagua viongozi wasiokuwa na anuani,” alisema Mnyeti
Awali, ofisa mtendaji wa kata ya Measkron Mwajuma Kipengele akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo alisema ilifunguliwa mwaka 2005.
Kipengele alisema shule hiyo ina wanafunzi 500 na wanafunzi 23 ambapo wananchi kwa kushirikiana na kamati ya maendeleo walijenga vyumba viwili kuanzia msingi hadi lenta.
Alisema katika sh35.9 milioni za ujenzi huo serikali kuu imechangia sh25 milioni na michango ya wananchi ni sh10.9 milioni.
Alisema wanakabiliwa na changamoto ya maabara kwani somo la kemia na fizikia hazijakamilika na wana ukosefu wa mabweni na maji.
Alisema pia wana uhaba wa walimu wawili wa somo la baiolojia na upungufu wa nyumba 20 za walimu.
Mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo, John Aloyce alisema wamejiandaa ipasavyo kuchagua viongozi wa serikali za mitaa watakaosimamia maendeleo ya eneo hilo.