Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi leo akiwa mkoani Simiyu amehudhuria matukio mawili ya Ufungaji wa Kambi ya Mafunzo kwa wanafunzi wa kidato cha Nne na Mkutano wa Chama cha Walimu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, iliyofanyika Mkoani Simiyu.
Mkutano huo wa siku mbili (Tarehe 30 hadi 31 Oktoba) umeandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), umehudhuriwa na walimu kutoka mikoa ya Kigoma, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita, Mara, Tabora na Kagera
Awali, wakati wa ufungaji wa Kambi ya Mafunzo Dkt. Abbasi alisema kupitia kambi hiyo ni matumaini yake kuwa watapatikana viongozi mahiri wa baadaye wa nchi hii na Serikali itaendelea kuunga mkono ili kuhakikisha wanafunzi katika kambi hizo wanaotoka kwenye familia ambako wanashindwa kujiandaa vema na wengine wanachangamoto mbalimbali za kielimu inakuwa chachu ya kuwasaidia kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.
Aidha, Dkt. Abbasi alimshauri Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, kuandaa kambi hizo kwa kuwapeleka siku moja moja wanafunzi hao kwenye kampasi za vyuo vikuu ili kuwajengea hamasa kwa wanafunzi hao katika kufanya vizuri zaidi katika masomo yao na kufika vyuo vikuu.
Katika hatua nyingine, akizungumza katika Mkutano wa Chama cha Walimu Tanzania, Dkt. Abbasi alisema kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za walimu ikiwemo kupandishwa madaraja na kulipa madeni yao kwani Muongozo wa Serikali wa sasa, ni kuwa madeni yasivuke mwaka wa Serikali na kwa sasa tayari fedha nyingi zimetolewa kwa ajili ya kulipa madeni ya walimu, watumishi wengine na hata sekta binafsi.
Ametoa mfano ambapo katika mwaka huu wa fedha pekee kati ya Julai na Septemba, 2019, tayari Shilingi Bilioni 85 zimetolewa kulipa madeni mbalimbali.
Dkt. Abbasi aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa walimu.
Ameeleza pia kuwa tayari wafanyakazi wa umma wapatao 306,000 wameshapandishwa madaraja na wengine wataendelea kupandishwa katika mwaka huu wa fedha.
Aidha, Dkt. Abbasi alisema kuwa Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa kiuchumi, ndio maana kuna utekelezaji wa miradi mikubwa kama mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere, na mradi wa reli ya kisasa.
Ameeleza kuwa miradi hiyo na ununuzi wa ndege ni ya kimkakati na inalenga kuwaandalia Watanzania nchi bora zaidi ijayo.
Vilevile, Dkt. Abbasi amesema Serikali imehakikisha wananchi wanapata taarifa kwa wakati, na ndio maana imetungwa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa mwaka 2016, ili kuruhusu kila mwananchi kufahamu mambo mbalimbali yanayoendelea