Mratibu wa mradi wa utetezi dhidi ya mila potofu na udhalilishaji wa kijinsia kutoka Asasi isiyokuwa ya Kiselikari ya Save Mother and Children of Central Tanzania (SMCCT) ya mkoani Singida, Evaline Lyimo akizunguza na wanafuzi wa Shule ya Msingi Mapambano wakati wa kutathmini mradi huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
ASASI isiyokuwa ya Kiselikari ya Save Morther and Children of Central Tanzania (SMCCT) ya mkoani Singida imeanza kufuatilia kesi ya ubakwaji wa mwanafunzi mwenye umri wa miaka nane wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mapambano ambapo mtuhumiwa wake aliachiwa huru.
Hatua ya asasi hiyo kufuatilia kesi hiyo ilitokana na kazi nzuri ya wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mama na mtoto na klabu ya wanafunzi ya kupinga vitendo vya ukatili mashuleni iliyoundwa na asasi hiyo katika shule hiyo kuibua tukio hilo ambapo mtuhumiwa alikamatwa na kuachiwa katika mazingira ambayo hayaeleweki baada ya kupelekwa kituo cha polisi cha Wilaya ya Ikungi huku wazazi wa mtoto huyo wakipigwa na bumbuwazi.
Akizungumza katika kampeni maalumu ya siku sita ya kupinga vitendo hivyo na tathmini ya mradi wa utetezi dhidi ya mila potofu na udhalilishaji wa kijinsia, mratibu wa mradi huo kutoka asasi hiyo, Evaline Lyimo alisema wamesikitishwa na kitendo cha mtuhumiwa huyo kuachiwa katika mazingira ambayo hayaeleweki na kuacha zimanzi kwa familia ya mtoto huyo hasa mama yake.
” Wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mama na mtoto na klabu ya wanafunzi ya kupinga ukatiki wa kijinsia tulioziunda ndio zilifanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo mtu mzima lakini tulishangaa baada ya kuona ameachiwa huku mtoto akibaki na maumivu ya kubakwa” alisema Lyimo.
Alisema tayari wamekwenda kuonana na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo na mkurugenzi wa wilaya hiyo ambao wameahidi kulifuatilia suala hilo na kulitolea majibu.
Mama mzazi wa mtoto huyo akizungumza mbele ya viongozi wa asasi hiyo waliokuwa katika kampeni hiyo ambayo imefadhiliwa na Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) inayolenga kutokomeza ukeketaji, ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni dhidi ya watoto alisema anaviomba vyombo vya dola wilayani humo kuhakikisha anapata haki ya suala hilo.
“Tumeachwa njia panda hatujui tuanzie wapi na tunashangaa kumuona mtuhumiwa akiwa nje na kila tukienda kuulizia kesi pale kituoni hatupati majibu ya kueleweka na ni miezi miwili sasa imepita tangu mtoto wangu afanyiwe kitendo hicho porini wakati akirudi nyumbani akitoka shule akiwa na wenzake waliofanikiwa kukimbia wakati mtuhumiwa huyo alipokuwa akimfanyia unyama huo” alisema mama huyo ambaye jina lake tunalihifadhi.
Mratibu wa mradi huo, Evaline Lyimo alisema katika kampeni hiyo shirika hilo lilitembelea kata sita na vijiji 18 pamoja na shule 25 zilizopo wilayani humo pamoja na kutathmini mradi huo ambapo waliwatembelea wahanga wa matukio ya ukatili kama kukeketwa, kubakwa, kulawitiwa na wale ambao wamerudishwa shuleni baada ya kupatiwa elimu na shirika hilo.