********************
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetumia Maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani kwa kutoa elimu, kusikiliza changamoto za wenye viwanda, wazalishaji na wajasiriamali na kuzipatia ufumbuzi ili kuhakikisha wanaendelea kufanya uzalishaji kwa kufuata mifumo sahihi.
Maofisa hao walikutana na wadau hao mwishoni mwa wiki katika ofisi za SIDO, Vingunguti jijini Dar es Salaam ambapo pia waliwahamasisha kushiriki katika uandaaji viwango.
Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) ambalo TBS ni mwanachama, huadhimisha Siku ya Viwango Duniani kila mwaka Oktoba 14, lakini kwa Tanzania kutokana na siku hiyo kuangukia tarehe ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, TBS ilisogeza mbele maadhimisho hayo hadi kuanzia Oktoba 21 na yanatarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 31, mwaka huu.
Ofisa Viwango Mwandamizi wa TBS, Joseph Mwaipaja, alisema wanatumia fursa hiyo kumbusha wadau umuhimu wa viwango, lengo likiwa ni kupunguza bidhaa zisizofaa katika masoko ya Tanzania na kuwajengea wananchi, wenye viwanda na wazalishaji uelewa wa pamoja kuhusiana na masuala ya viwango.
“Unapotengeneza bidhaa, wewe ndiye unayefahamu vizuri zaidi bidhaa yako, kwa hiyo ni muhimu kujumuisha matakwa ya wenye viwanda kwenye viwango vyetu,” alisema Mwaipaja.
Alisema maofisa wa shirika hilo walienda SIDO ili kuwakumbusha wenye viwanda na wajasiriamali kuwa bidhaa wanazozalisha lazima zikidhi vya viwango kitaifa.
Mwaipaja alisema mwaka huu wanaadhimisha siku ya viwango wakijivunia kuendelea kuenea kwa elimu ya viwango kwa kasi miongoni mwa Watanzania wengi, kwani bidhaa nyingi zinazozalishwa sasa ni zile zinazokidhi viwango.
Alifafanua kuwa Rais John Magufuli anasisitiza ujenzi wa Tanzania ya viwanda, hivyo na wao lazima wamsaidie ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, alisema kuanzia Oktoba 21 hadi 31, mwaka huu kuna mambo ambayo yameamua kuyafanya ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani.
Alisema wamekuwa wakitoa elimu ya viwango kwa njia mbalimbali kwa kushirikiana na vyombo vya habari na wameona elimu ni muhimu zaidi kuanzia chini.
Ili kueneza elimu hiyo ya viwango katika kipindi hiki cha maadhimisho hayo, Mtemvu alisema watatembelea shule 12 za msingi na sekondari kwa ajili ya kutoa elimu ya viwango na umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora.
Mtemvu aliongeza kwamba wameona kuna umuhimu wa kukutana na wadau wao, ndiyo maana walienda SIDO kukutana na wazalishaji wenye viwanda, kwani pamoja na changamoto zilizopo wanatambua mchango wao katika kuendeleza viwango.
“Wadau wanaposhiriki katika uandaaji viwango inatusaidia kama taifa kupata viwango ambavyo vinatekelezeka,” alisema Mtemvu.
“Tumekuja hapa kuongea nao, tutawatembelea, tutawafundisha na tutawahamasha washiriki kwenye uandaaji wa viwango.” Alisema.
Alisisitiza kuwa wao kama shirika wameona washiriki maadhimisho hayo kwa namna hiyo ili mwisho wa siku wanafunzi, wananchi na wadau wawe na uelewa wa pamoja kuhusu viwango.