Home Mchanganyiko DKT.KAWAMBWA ATOA MIL.30.8 ZA MFUKO WA JIMBO KUPIGA TAFU VIKUNDI 30 VYA...

DKT.KAWAMBWA ATOA MIL.30.8 ZA MFUKO WA JIMBO KUPIGA TAFU VIKUNDI 30 VYA UJASIRIAMALI

0

****************************

NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
MBUNGE  wa Jimbo la Bagamoyo,Dkt Shukuru Kawambwa amekabidhi sh.milioni 30.801 kwa vikundi 30 vya wajasiriamali wanawake, vijana na wazee ili ziwasaidie katika shughuli zao za ujasiriamali.
Hafla ya kukabidhi fedha hizo ambazo ni ruzuku toka mfuko wa Jimbo, imefanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo ambapo wawakilishi wa vikundi vilivyonufaika vimekabidhiwa fedha hizo ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo kugawa fedha za mfuko wa jimbo kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo kwa ajili ya kuchochea maendeleo kwenye shughuli za kiuchumi wanazofanya.
“Katika ugawaji wa fedha hizi kila kikundi kimeangaliwa vizuri, vikundi vya vijana, wazee na wanawake, hakukuwa na ubaguzi, lengo likiwa ni kuhakikisha tunawafikia walengwa na kuwasaidia kuzifikia ndoto zao kwa kuwawezesha kidogo ili kujiinua kiuchumi” alieleza Kawambwa.
Aliongeza baada ya ugawaji wa fedha hizo, atashirikiana na madiwani na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo, kuwatembelea wanavikundi hao ili kuona kama fedha zilizotolewa zimekwenda kufanya kazi iliyokusudiwa.
Aliwahamasisha wananchi wa Bagamoyo, kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali vya wanawake, wenye ulemavu na vijana katika maeneo yao.
“Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, imetenga sh.211.915  toka mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na wenye ulemavu, robo ya fedha hizi hutolewa mara moja kila baada ya miezi 3,”
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Fatuma Latu ,alifafanua kwa miaka minne mfululizo mfuko wa Jimbo la Bagamoyo, umekuwa ukitoa wastani wa sh. milioni 30 kwa taasisi za serikali na vikundi vya wajasiriamali wadogo ndani ya halmashauri.
Mmoja wa wanufaika wa ruzuku hiyo ya mfuko wa Jimbo, mzee Golden Mwenda, toka kikundi cha Unjacha kilichopo Chasimba, Kata ya Yombo, ambao wanajihusisha na kilimo cha muhogo, amepongeza hatua hiyo ya utoaji fedha za ruzuku kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo ambazo zitawawezesha kuinua biashara zao.