Mratibu wa Mradi Mpya wa Maji Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Doris Mulashani, akifungua warsha ya mafunzo ya uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa mradi utakaokwenda sambamba na malipo kutokana na matokeo chanya ya kazi uendelevu, usambazaji wa maji na usafi wa mazingira vijijini.
Mwakikishi wa Benki ya Dunia katika warsha hiyo, Toyoko Kodama akiwasilisha mada.
Wadau wa maji wakiwa katika warsha hiyo.
Majadiliano yakiendelea katika warsha hiyo.
Majadiliano katika makundi yakiendelea.
Na Dotto Mwaibale, Singida
BENKI ya Dunia imetenga dola za marekani milioni 350 zitakazotumika kulipia ujenzi mpya wa mradi wa maji utakaokwenda sambamba na malipo kulingana na matokeo ya kazi (PforR).
Hayo yalielezwa jana na mratibu wa mradi huo, Mhandisi Mashaka Sitta wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye warsha ya mafunzo ya uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa
mradi huo inayofanyika mjini Singida.
“Tayari sh.166 bilioni zimekwisha tolewa kama mbegu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu kwa mikoa 17 na halmashauri za miji 86″ alisema Sitta.
Alisema tayari wameanza kutoa mafunzo ya uelewa wa pamoja kwa watendaji ili kukidhi vigezo vya namna ya kupata fedha hiyo na utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi.
Alisema mafunzo hayo wameanza kuyatoa katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Singida na wanatarajia kwenda Mwanza lengo likiwa ni kuelewa viashiria na mahitaji ya mradi.
Sitta alisema kila wilaya wanatarajia kupeleka sh.1. 36 bilioni na kuwa kila mwaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) itafanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo.
“Azma iliyopo pamoja na mambo mengine ni kutatua kabisa changamoto za maji, elimu na afya hapa nchini” alisema Sitta.