Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam Badru Idd (wa pili kulia) akiwaongoza wenzake kuchangia damu katika Hospitali ya Ocean Road.
…………………………………………………
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inakabiliwa na uhaba wa damu hali inayosababisha wakati mwingine huduma kushindwa kutolewa kwa ufanisi.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Ocean Road, Dk. Mark Mseti, amesema kwa siku za hivi karibuni hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa damu hali inayokwamisha utoaji huduma kwa wahitaji.
Mseti alisema mahitaji ya damu katika hospitali hiyo ni makubwa kutokana na tiba zote za mionzi kuhitaji wagonjwa kuwa na damu ya kutosha ili ziweze kufanya kazi sawasawa .
“Tunahitaji chupa za damu 40 hadi 50 kila siku, kuna wakati Mpango wa Taifa wa Damu Salama unaileta kwa kiwango kinachostahili tunapata chupa 50 au 40 na tunaweza kufanya kazi kama inavyostahili lakini hivi karibuni kwa takribani wiki mbili hivi kumetokea uhaba mkubwa wa damu kwenye taasisi yetu. Kwa mfano jana na juzi tulipata chupa zisizozidi 20 kwa siku,” amesema Dk Mseti.
Katika kujaribu kukabiliana na changamoto hiyo wafanyakazi wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam wametumia huu mwezi wa Huduma kwa Wateja kwa kuchangia uniti 97 za damu.
Dk. Mseti amesema kiasi hicho cha damu kitatumika kwa wagonjwa 240 wenye uhitaji wa tiba hiyo.
Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, amesema lengo la kushiriki zoezi hilo ni kuangalia jinsi ya kuokoa maisha ya watanzania wenzao wenye uhitaji.
Amesema kupitia zoezi hilo walilolifanya,anatoa rai kwa Watanzania wengine kushiriki kuokoa maisha kwa kuchangia damu
“Nimetembezwa hospitalini unakuta hata hiyo damu inayohitajika haipo au ni kidogo, watanzania tujitolee kuokoa maisha ya wenzetu,” amesema