Na Jozaka Bukuku
TAKWIMU ya Sensa ya watu na makazi ambayo ilifanyika mwaka 2012 ilionesha
kuwa Tanzania kuna jumla ya wakazi wasiopungua milioni 47.4 Bara na Visiwani.
Katika idadi hiyo utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014 ulionesha vijana ni asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa.Wastani huo unawagusa vijana wenye rika la kuanzia umri wa miaka 18-35 kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2007.
Tafiti hizo zinaashiria kuwa tabaka la vijana ndio tegemezi kwa uzalishajimali na
kutengeneza pato la Taifa.Vijana wanachukuliwa kuwa chachu ya kuchochea
maendeleo ya Nchi.
Lakini pamoja na hayo, vijana walio wengi nchini bado wanasumbuliwa na
changamoto za ajira na hasa kwenye sekta zilizo rasmi.Inakadiriwa kuwa kila
mwaka vijana wanaohitimu elimu ya msingi, sekondari na vyuo wanafikia milioni
moja ambapo katika hao ni vijana wasiozidi 40000 wanaopata ajira rasmi.
Hii ina maana kuwa soko la ajira bado halijaweza kukidhi haja ya vijana
wanaowania nafasi mbalimbali za kazi baada ya kuhitmu masomo yao.
Zipo jitihada mbalimbali ambazo zinachukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na
wadau wa Sekta binafsi ili kuweza kuondokana na tatizo hili sugu ikiwemo elimu
ya ujasiriamali,mikopo, ruzuku na kurasimisha biashara za vikundi vya uzalishaji
mali.
Moja kati ya Taasisi binafsi zinazounga mkono jitihada za Serikali kuondoa tatizo la ajira ni pamoja na Taasisi ya TGT (Tanzania Growth Trust) ambayo imejikita katika kutoa mafunzo ya uzalishajimali kwa nadharia na vitendo,kutoa mikopo yenye mashari nafuu kwa makundi ya wanawake , vijana na watu wenye ulemavu, kusimamia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa masoko ya kisasa ikiwemo soko la Mburahati jijini Dar es salaam n.k.
Akizungumza kuhusiana na mikakati ya Taasisi hiyo,Afisa Mtendaji Mkuu wa
Taasisi hiyo Bibi Anna Dominick amesema kwamba Taasisi yake inafahamu
ukubwa wa changamoto ya ajira kwa vijana ndio sababu haswa ya kutoa mafunzo ya nadharia kwa vikundi vya uzalishajimali na baada ya kufuzu wanawaunganisha na fursa za mikopo yenye masharti nafuu.
“Tumekuwa na programu nyingi katika taasisi yetu lakini kwa kiasi kikubwa vijana ambao wamekuwa wakinufaika na mikopo kutoka TGT huwa tuna utaratibu wa kuwapitisha kwenye hatua za mafunzo ili kuhakikisha wanazalisha bidhaa zilizokuwa bora na kurasimisha biashara zao kutoka kwenye mamlaka
husika”alisema Bibi Anna Dominick.
“Tunafanya kazi hii kwa ushirikiano na mamlaka za Serikali ambapo wadau kama SIDO, TRA, TFDA na TBS tumekuwa tukiwaalika ili kuwafunza vijana namna ya kurasimisha biashara zao kabla ya kuziendea taasisi za kifedha ili kupata mikopo”aliongeza Afisa Mtendaji Mkuu huyo.
Bibi Anna alimalizia kwa kusema kwamba mwishoni mwa mwezi huu TGT
imepanga kufanya Kongamano kubwa Mkoa wa Pwani ambalo litakuwa na lengo
la kutoa mafunzo ya ujasriamali kwa makundi ya wanawake,wakulima na kada
zingine za wazalishajimali.
Dira ya Taifa kwa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha Tanzania inafikia
uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ambayo ina uhusiano wa moja kwa moja
na masuala ya kilimo.Jitihada hizi zimeanza kuzaa matunda kutokana na uungwaji
mkono ambao unatolewa na sekta binafsi kwa Serikali.