Home Mchanganyiko Wasaidizi wa msaada wa kisheria Iringa waomba ushirikiano

Wasaidizi wa msaada wa kisheria Iringa waomba ushirikiano

0

**********************************

Na Francis Godwin ,Iringa

Wasaidizi   wa  msaada  wa  kisheria mkoani  Iringa  wametaka  kutambuliwa na vyombo  mbali  mbali  vya  kisheria  kama  polisi ,mahakama  na magereza  ili  kuepuka  kusumbuliwa pindi  wanapotekeleza  majukumu yao ya  kuhudumia jamii .

Wakizungumza jana   katika  ukumbi  wa  siasa ni kilimo katika mdahalo  wa siku  moja    juu ya sharia za msaada  wa kisheria Tanzania ,utekelezaji  wake ,changamoto  na mafanikio yake ,   washiriki  wa mdahalo  huo  walisema  kuwa  kutokana na kutotambuliwa kumekuwepo na usumbufu  mkubwa kwa baadhi ya  wasaidizi wa  kisheria  kukamatwa ama  kuzuiliwa  kutoa  huduma katika jamii .

Msaidizi wa  kisheria   kutoka  Halmashauri ya Mufindi Gabriel Nsemwa alisema   kuwa  wasaidizi  hao  wamekuwa  wakishindwa  kutimiza  wajibu  wao  hasa pale  wanapokutana na polisi  katika maeneo ya wao kufuatilia matukio yanayohitaji  msaada  kutoka kwao .

Alisema  kuwa  mwezi  uliopita  msaidizi wa kisheria  mwenzake  kutoka  wilaya ya Mufindi  akiwa katika utekelezaji wa majukumu yao alikutana na  polisi ambao  walimkamata na  kumpeleka   kituo  cha polisi na kukaa ndani kwa masaa nane .

“ Huyu  alikamatwa  usiku  wakati  akifuatilia  tukio ambalo  lilikuwa likihitaji msaada na akiwa  eneo la tukio  polisi  nao  wakiwa katika ufuatiliaji wa tukio  hilo  hilo  walimkamata na  kumpeleka kituoni Mafinga  na  kutozwa  faini ya shilingi 230,000 na  kukaa mahabusu masaa nane  kuwa hawamtambui kama msaidizi wa kisheria  hivyo  tunataka  kujua  uhakika wa usalama  wetu  pindi  tukiwa katika utekelezaji wa majukumu yetu “

Kuwa  ili  kuepusha   kukamatwa kwa  watoa huduma   za  kisheria na polisi ni  vizuri  chama  cha mawakili Tanganyika   kuangalia  uwezekano wa  kuwalinda ili  wasiendelee  kunyanyasika  wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao .

 Kwa  upande  wake mkaguzi  msaidizi wa polisi Elizabeth Swai  ambae  alimwakilisha mkuu wa  upelelezi  wa  polisi kwenye  mdahalo  huo  alisema  kuwa  ni  vizuri  kwa wasaidizi hao  wa  kisheria na  mawakili  kufanya kazi  kwa  kufuata  taratibu za  sehemu  husika badala ya  kutaka  kuingia hata maeneo ambayo hawapaswi kuingia  bila  ruhusa  ya utawala wa eneo  mfano mahabusu .

Kwani  alisema wapo  baadhi ya  mawakili ama  wasaidizi wa  kisheria wamekuwa  wakilamisha kuingia mahabusu  kutaka  kuongea  na mahabusu bila  kufuata taratibu jambo  ambalo si sawa  kwani  kama  watafuata  taratibu  hakuna  askari atakayezuia wakili ama  msaidizi wa  kisheria  kufanya mazungumzo na mahabusu .

Katibu  mkuu wa shirika la LREO  Jimmy Mgovano  alisema  kuwa  ili  kuepuka  wasaidizi wa  kisheria kutonyanyasika  katika maeneo ya  mahakama ,polisi ama magereza  ni vizuri kukawa na orodha  ya  wasaidizi wa  kisheria  wote  ndani ya  mkoa ambao  majina yao  yatakuwepo kila eneo ili  wakifika  waweze  kutambuliwa kwa orodha   hiyo .

Mratibu  wa chama  cha mawakili mkoa wa Iringa  Omary Sarehe alisema  kuwa   kila mwaka  chama  cha  mawakili Tanganyika   wamekuwa  wakiandaa  wiki ya  msaada  wa  kisheria  kwa  ajili ya  kuwatambua  watu  wenye  uhitaji wa msaada wa  kisheria katika vyombo  vya  kisheria  hasa mahakamani .

 Hivyo  alisema  kuwa   ni  vema  serikali  kuanzisha  utaratibu  wa  kuandaa  orodha  ya  wasaidizi wa  kisheria  wote  ambayo itakuwepo kila idara  ili  kuepuka  tasnia  hiyo  kuingiliwa na mawakili makanjanja.

Japo  alisema  kuwa upande wa mahakama  wamepiga hatua kwa kuanzisha  mfumo  wa   kimtandao  ambao  unatambua   mawakili  wote  na  wananchi  wanaweza  kukwepa  kutapelewa na mawakili  feki  kwa  kutembelea  katika mtandao na  kutafuta  mawakili  ambao wanatambulika