******************************
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
24.10.2019
SERA ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003, pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya Serikali kutumia fursa za TEHAMA katika utendaji kazi wa kila siku na utoaji huduma kwa wananchi.
Katika kutekeleza sera hiyo, mwaka 2004 Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma (OR-MUU) ilianza kuchukua hatua mbalimbali kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kuimarisha mifumo ya utoaji habari na huduma kwa wananchi.
Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kuanza utekelezaji wa dhana ya Serikali Mtandao iliyokuwa sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Mabadiliko katika Utumishi wa Umma (Public Service Reform Programu – PSRP).
Programu hiyo ililenga kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na uboreshaji wa utoaji huduma kwa umma. Pamoja na mambo mengine, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ziliwezeshwa kuwa na mifumo imara ya Menejimenti ya Habari.
Aidha, Serikali iliziwezesha taasisi za umma kuwa na Tovuti zake ambapo hadi kufika mwaka 2010 takribani Taasisi zote za Serikali zilikuwa na Tovuti, ambapo kwa sasa matumizi ya TEHAMA yameongezeka kwa kasi Serikalini na zimeongeza uwazi, ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika anasema Serikali imeendelea kusimamia matumizi ya mifumo na miundombinu ya TEHAMA Serikalini ili kuongeza ufanisi na usalama wa taarifa za Serikali.
Anaongeza kuwa mifumo na miundombinu hiyo ni pamoja na Vituo Vikuu vya Kuhifadhi Mifumo na Taarifa za Serikali kwa kuongeza Taasisi mpya 13 hivyo kufanya jumla ya taasisi zilizohifadhi mifumo na taarifa zao kufikia 43, Mfumo wa barua pepe Serikalini (GMS) kwa kuongeza taasisi mpya 39 na kufanya jumla ya taasisi zilizounganishwa kufikia 398.
Anaitaja mifumo na miundombinu mingine ni Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-office) kwa kuongeza taasisi mpya 15 na kufanya jumla ya taasisi zilizounganishwa kufikia 48, Mfumo wa kutoa huduma kwa Umma kupitia simu za Mkononi (Government Mobile Platform (GMP) kwa kuongeza taasisi mpya 24 na kufanya jumla ya taasisi zilizounganishwa kufikia 146.
Kwa mujibu wa Mkuchika anasema Serikali ilitoa mafunzo ya utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa kwa Viongozi, Wasimamizi wa TEHAMA na watumiaji wa huduma za Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma 98 ili kuongeza uelewa na uwezo wa Taasisi hizo katika kutumia TEHAMA, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri Mkuchika anasema Serikali pia ilitoa ushauri wa kitaalam kwenye maeneo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma 23 ili kuhakikisha kwamba uwekezaji unaofanywa na Serikali kwenye TEHAMA unatoa matokeo yaliyokusudiwa.
‘‘Msaada wa kiufundi umetolewa kwa Taasisi za Umma 252 kupitia Mfumo wa Kutoa Msaada na Huduma kwa Wateja (Helpdesk System) unaopatikana saa ishirini na nne (24/7)’’ anasema Waziri Mkuchika.
Akifafanua zaidi Waziri Mkuchika anasema Mifumo mikubwa ya TEHAMA imetengenezwa kwa Taasisi za Umma kwa lengo la kuboresha utendaji kazi, kuboresha utoaji huduma kwa umma, kurahisisha ukusanyaji wa mapato na kuondoa mianya ya rushwa.
Anaitaja baadhi ya mifumo iliyotengenezwa ni pamoja na Mfumo wa Tiketi za Kieletroniki kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Mfumo wa kusajili wahandisi kwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Mfumo wa kufanya usajili wa wataalam wa ununuzi na ugavi kwa Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).
‘’Wataalam wa Wakala ya Serikali Mtandao 11 wamewezeshwa kupata mafunzo yanayotolewa na Bodi mbalimbali za Kitaalam kwenye maeneo ya usalama mtandao, miundombinu na utengenezaji wa Mifumo na Vile vile watumishi 7 wamewezeshwa kupata mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Stashahada, Uzamili na Uzamivu’’ anasema Waziri Mkuchika.
Matumizi ya TEHAMA yameisaidia Serikali kuongeza uwazi, ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi hususani katika zama hizi ambazo taarifa na huduma za Serikali zimekuwa zikitolewa kwa njia ya nyaraka kupitia muundo wa karatasi.