Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Selemani Jafo amesema kuwa Kuna halmashauri 121 hazikufikia lengo walilowekewa la kuhakikisha wanakusanya zaidi ya asilimia 25 ya makisio yake.
Huku bajeti iliyoidhinishwa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mwaka huo ni sh. Bilioni 765.48, huku robo ya kwanza July hadi Septemba,2019, Halmashauri zimekusanya sh. Bilioni 166.24 sawa na asilimia 22 ya makisio ya mwaka.
Waziri Jafo ameyabainisha leo Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya mapato ya vyanzo vya ndani vya halmashauri kwa kipindi Cha Julai Hadi Septemba kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Amesema halmashauri zote zilitakiwa kukusanya mapato kwa asilimia 25 ya makisio yake ya mwaka, hata hivyo kuna halmashauri zipatazo 121 hazikuweza kufikisha asilimia 25, wakati zilizofikia lengo zikiwa 54 tu.
“Nitoe salamu kwa Wakurugenzi na huu ni ujumbe mwingine msione kwa wenzenu waliopita, niwaambie ukusanyaji wa mapato ndio kigezo kinachowafanya mkae kwenye nafasi zenu, mmeteuliwa kusimamia mapato” amesema Jafo.
Amewataka kutumia mwezi Oktoba hadi Disemba kujitathmini na kuhakikisha Wakurugenzi hao wanafikia malengo waliyowekewa na kufikisha asilimia 25 za makisio yao.
Pia amewaonya Wakurugenzi wote wazembe ambao wanasuasua kwenye ukusanyaji wa mapato na kutaka wajitathmini kwa miezi mitatu ijayo
Ameongeza kuwa ” Mkurugenzi wa Buhigwe anapaswa kujitathmini na naomba Katibu Mkuu uliweke vizuri kwa sababu nilienda Buhigwe hata utekelezaji wa miradi ya maendeleo unasuasua, hata miradi iliyopelekewa fedha na Serikali kuu” amesema.
Kuhusu hali ya ukusanyaji, Waziri Jafo amesema Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imekuwa ya kwanza kiasilimia kwa kuwa imekusanya imekusanya mapato kwa asilimia 52 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka huu, huku halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya asilimia 3 ya makisio yake.
Wakati Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza kwa makusanyo ya mapato mengi zaidi kuliko halmashauri zote kwa kukusanya Bilioni 13.10, huku halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya sh.milioni 35.15.
Aidha Waziri Jafo amebainisha kuwa Mkoa wa Dar es saalam umeongoza kwa wingi wa mapato ambapo umekusanya Bilioni 39.53, huku Mkoa wa Kigoma ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya Bilioni 2.12 katika kipindi hicho.