Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)

 

Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo, Kilimanjaro

 

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo

inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)

ambayo ni utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Nchini

(TASFIP) unaolenga kukuza kilimo kwa asilimia 6 kwa mwaka.

 

Kwa kuzingatia hatua hizo, Wizara ya

Kilimo imekusudia kuleta mageuzi ya kilimo kutoka mtazamo uliopo wa kilimo cha

kujikimu hadi kufikia uendeshaji wa kilimo kwa mfumo wa kibiashara.

 

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga

(Mb) ameyasema hayo leo Tarehe 21 Octoba 2019 wakati akizungumza kwenye

ufunguzi wa Programu ya kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani pamoja na

uzalishaji bora wa mazao ya viungo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa

Hotel ya Uhuru Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.

 

Mhe Hasunga ameyataja maeneo ambayo yanahitaji utekelezaji wa haraka. Mosi, Utekelezaji wa adhma ya serikali

kuendeleza kilimo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya

Pili (ASDP II) kwa kusimamia thabiti nguzo ya programu hiyo

ikiwemo Usimamizi endelevu wa matumizi ya maji na ardhi.

 

Alisema kuwa Lengo la ASDP II ni kuleta

mageuzi katika  Sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija, kilimo

cha kibiashara, kuongeza pato kwa wakulima hivyo nilazima kuwekwa mkakati

madhubuti wa utekelezaji ili kufikia nalengo yaliyokusudiwa.

 

Vilevile, alisema kuwa serikali

imekusudia Kuboresha mazingira wezeshi, uratibu, ufatiliaji na tathmini katika

sekta ya kilimo hivyo wataalamu katika Wizara ya kilimo wanapaswa kuongeza kasi

ya uwajibikaji ili kutimizi adhma hiyo.

 

Alisema Wizara ya kilimo itaweka

mkakati madhubuti wa kuhakikisha kuwa bei ya Mazao inaimarika huku akisisitiza

kuwa kwa ushirikiano na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji atahakikisha

wakulima wanapata masoko ya mazao yao.

 

Amesema kuwa Wizara ya Kilimo imetayarisha Mkakati wa Taifa wa miaka 10 wa Usimamizi wa Mazao baada ya kuvunwa.

 

Alisema kuwa mkakati huo umeandaliwa ili kuendana na malengo endelevu ya Dunia ya kutokomeza njaa ifikapo 2030, kuhakikisha usalama wa chakula na lishe na kukuza kilimo endelevu kama lengo la pili la Umoja wa Mataifa kati ya Malengo 17.

 

Mkakati huo utakuwa Mwongozo kwa Sekta za Umma na Binafsi katika kukabiliana na changamoto ya upotevu wa Mazao baada ya mavuno. Aidha, Mkakati huo umezingatia mabadiliko yanayoendelea ya Kitaasisi na Kisera.