KLABU ya Azam FC leo imemtambulisha Mromania, Aristica Cioaba kuwa tena kocha wa timu hiyo akichukua nafasi ya Mrundi, Etienne Ndayiragije ambaye anakwenda kuwa kocha wa kudumu wa Taifa Stars.
Aristica ambaye awali aliiongoza Azam FC msimu wa 2017–2018, anajiunga tena na klabu hiyo akitokea Sohar SC ya Oman.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema kwenye mkutano na Waandishi kwamba Cioaba anachukua nafasi ya Ndayiragije ambaye anahamia Taifa Stars moja kwa moja.
“Tunayofuraha kubwa kuwafahamisha kuwa tumeingia mkataba wa mwaka mmoja na Kocha wetu wa zamani Aristica Cioaba. Kocha huyo raia wa Romania, aliyewahi kuinoa Azam FC misimu miwili iliyopita, ataanza majukumu yake mara moja tutakapokamilisha taratibu za vibali vyake vya kufanya kazi nchini,”amesema Popat.
Aidha, Popat amesema kwamba ilivyokuwa awali Cioaba, mwenye leseni ya juu ya ukocha ya UEFA Pro, amerejea sambamba na Kocha wa viungo, Costel Birsan, aliyekuwa naye awali kipindi anaifundisha Azam FC.
Mara baada ya kuingia mkataba rasmi mapema leo Jumatatu, Cioaba ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi na uongozi mzima wa Azam FC kwa kuendelea kuwa na imani naye. “Naushukuru uongozi wa Azam FC kwa kuendelea kuwa na imani na mimi, kikubwa mimi sio mgeni hapa naijua timu, wachezaji wananijua na pia wanafahamu falsafa yangu, jambo kubwa ni kuendelea kuifanya timu kuwa juu pamoja na kushinda mataji,” alisema.
Ndayiragije anaenda timu ya Taifa, baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC kuridhia ombi la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanaomuhitaji awe kocha mkuu wa kudumu baada ya kufanya vizuri akiwa na kikosi hicho akiwa kocha wa muda.
“Azam FC tunamtakia kila la kheri, Ndayiragije katika majukumu yake mapya akiwa Taif Stars, ambapo tutakuwa naye sambamba pale atakapohitaji kutoka kwetu msaada kwenye masuala yake kiufundi,” amesema Popat.