TANZANIA imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwakani nchini Cameroon baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Sudan leo Uwanja wa Omdurman, Mourada mjini Omdurman.
Shujaa wa Tanzania leo alikuwa ni mshambuliaji Ditram Nchimbi aliyeongezwa kikosini baada ya mechi ya kwanza ambaye leo alisababisha bao la kwanza na kufunga la pili.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars inayofundishwa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragijje inafuzu CHAN ya 2020 kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla ya 2-2, kufuatia kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam.
Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Taifa Stars kufuzu fainali za michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, baada ya mwaka 2009 nchini Ivory Coast, ikiitoa Sudan pia katika raundi ya mwisho ya kufuzu.
Sudan ilitangulia kwa bao la Amir Kamal dakika ya 30 akimalizia krosi ya Ahmed Adam Mohamed aliyemlamba chenga beki wa kulia wa Tanzania, Salum Kimenya.
Nchimbi akaangushwa nje kidogo ya boksi na mabeki wa Sudan aliowazidi mbio na Nahodha, Erasto Edward Nyoni akaenda kufunga kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 49 kuisawazishia Taifa Stars.
Nchimbia aliyejumuishwa kikosini baada ya kufunga hat trick katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, timu yake Polisi ikitoa sare ya 3-3 na vigogo, Yanga SC akafunga bao la ushindi dakika ya 79 akimalizia pasi ya mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda.
Furaha zaidi ni kwa kipa mkongwe wa Tanzania, Juma Kaseja aliyerejeshwa kikosini baada ya miaka mitano, ambaye amedaka mechi zote za kufuzu na kuipa tiketi ya CHAN nchi yake.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Juma Kaseja, Salum Kimenya, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Bakari Kondo, Jonas Mkude, Miraj Athumani/Ayoub Lyanga dk64, Frank Domayo/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk82, Muzamil Yassin, Ditram Nchimbi na Iddi Suleiman ‘Nado’/Shaaban Iddi Chilunda dk62.