*************************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo amekabidhi gari la kubebea wagonjwa lililogharimu milioni 134 na gari jingine aina ya Toyota pickup la milioni 92 kwa mganga mkuu wa mji wa Kibaha.
Magari hayo yametolewa na halmashauri ya Mji wa Kibaha,ambapo yamenunuliwa kupitia wakala wa wanunuzi .
Akikabidhi gari hilo la wagonjwa kwa mganga mkuu wa Mji wa Kibaha,Tulitweni Mwinuka ,huko katika kituo cha afya mkoani, mkuu huyo alisema ni maamuzi muhimu kwani yatasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa gari la dharura.
“Sio litumike kubeba vitu vya magendo, maana wengine wanaweza kutumia vibaya wakiamini kila mmoja atakuwa hana hofu kwakua linajulikana linabeba wagonjwa” alisisitiza Ndikilo.
Wakati huo huo alitaja takwimu za siku ya kwanza ya chanjo ya surua Rubella Octoba 18 watoto 28,000 kati ya 163,900 Surua Rubella walipatiwa chanjo na Polio 19,000.
Ndikilo aliwataka baadhi ya wazazi na walezi kuacha visingizio vya hali ya hewa,na badala yake wajitokeze kwa wingi kupeleka watoto waliolengwa kupata chanjo ya Surua Rubella na Polio.
“Tuwakinge watoto hawa na magonjwa ambayo chanjo zinatolewa, tuondokane kabisa na magonjwa haya” alisema Ndikilo.
Mganga mkuu wa Mkoa Gunini Kamba alisema, kabla ya kuanza kwa kampeni, Surua ilikuwa chanzo kikubwa cha maradhi, ulemavu, utapiamlo na vivo vya watoto wenye umri wa miaka mitano.
Nae Mganga mkuu wa Mji wa Kibaha Tulitweni Mwinuka alisema, kwenye kampeni hiyo kwa mwaka huu Halmashauri hiyo imepangiwa watoto 16,629 wa chanjo ya Surua Rubella na Polio 10,757.