Viongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania wa Bara na Visiwani Zanzibar wakifuatilia majadiliano katika Mkutano na Viongozi kutoka Benki ya Dunia (hawapo pichani) uliofanyika Jijini Washington DC. Wa kwanza kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi na anayefuatia kulia kwa Mhe. Balozi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Mashimba Ndaki.
****************************
Na Eva Valerian na Ramadhani Kissimba, Washington DC
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatarajia kupata dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia-WB zitakazotumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya kukuza Utalii na kustawisha miji katika visiwa hivyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Khamis Omar alisema Jijini Washington DC kuwa Benki ya Dunia imekuwa mshirika mzuri wa maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutokana na misaada mbalimbali wanayoitoa katika kutekeleza miradi yao ya maendeleo.
Bw. Omar alisema Benki hiyo imesaidia kufadhili ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara zinazoingia mijini, Uwanja wa Ndege wa Zanzibar pamoja na bandari.
Aidha, alisema Benki hiyo imesaidia zaidi katika ujenzi wa Uwanja wa ndege, kwa kujenga sehemu ya maegesho ya ndege, njia ya kutua na kurukia ndege na njia ambazo ndege zinapita kabla ya kuingia kwenye sehemu ya kurukia (runway).
“Pia Benki hii imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya Elimu Visiwani Zanzibar ukiwemo mradi wa kukuza matokeo na kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika shule za Zanzibar” alisema Bw. Omar
Alieleza kuwa kwa sasa wanatekeleza mradi mkubwa wa ustawishaji wa huduma za mijini ambao unafadhaliwa na Benki ya Dunia, na mradi huo utasaidia kuboresha huduma muhimu katika Miji ya Zanzabar ikiwa ni pamoja na kuongeza vivutio vya utalii.
“Mradi huu umekamilika katika awamu ya kwanza,na awamu ya pili itatekelezwa baada ya Benki hiyo kuridhia na kutoa idhini ya utekelezaji wa mradi huo ambapo idhini hiyo inatarajiwa kutolewa mwezi Aprili, 2020” alisisitiza Bw. Omar
Katibu Mkuu -Wizara ya Fedha na Mipango ameishukuru Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa kwa ushikiano mzuri wanaouonyesha katika kusukuma maendeleo ya Visiwani Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla.
Awali Waziri wa Fedha na Mipango, wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Mohamed Abdiwawa alisema lengo la kushiriki katika Mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia-WB na Shirika la Fedha la Kimataifa -IMF ni kujadiliana na vyombo hivyo vya fedha duniani kuhusu miradi inayotekelezwa kwa sasa na kuangalia mustakabali wa utekelezaji wa miradi ambayo inategemewa kutekelezwa kwa siku zijazo.