*******************************
DAR ES SALAAM 18/10/2019
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo CP Liberatus Sabas, amefanya
doria ya angani katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuangalia
maeneo ambayo yamekumbwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha kwa siku za hivi karibuni.
Kamishna Sabas amesema kuwa, madhara yaliyotokana na mvua hizo ni
madogo ambapo maeneo ambayo makazi ya watu yamezungukwa zaidi
na maji ni maeneo ya Jangwani jijini Dar es Salaam sehemu ambayo tatizo
hilo hutokea mara kwa mara licha ya wakazi wa maeneo hayo kuamriwa
kuhama kwenye maeneo hayo.
Aidha Kamishna Sabas ameongeza kuwa katika maeneo ya Kimara
kumeripotiwa tukio moja la mtoto kufariki dunia jana baada ya kutumbukia
kwenye mkondo wa maji na juhudi za kutafuta mwili wake zinaendelea.
Katika Mkoa wa Pwani watu takribani 17 wameokolewa jana kutoka
maeneo hatarishi na kwenda maeneo salama ili kunusuru maisha yao. Pia
Kamishna Sabas ametoa angalizo kwa wakazi wote nchini wanaoishi
maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko wahame na kwenda maeneo
ambayo ni salama ili kuepukana na madhara ya mvua.
Katika hatua nyingine Kamishna Sabas ametoa wito kwa Watanzania
ambao bado hawajajiandikisha katika daftari la mpiga kura, kujiandikisha ili
kuweza kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na
kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha uchaguzi huo
unafanyika kwa amani kuanzia katika kampeni mpaka uchaguzi wenyewe.