Kundi la walimu wa Taasisi hiyo wakionesha umahiri katika tamasha la mwaka jana
Waziri Mwakye akijaribu fulana katika tamasha la mwaka jana huku Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Dk Herbert Makoye akifurahia hatua hiyo
**************************
>Wasanii zaidi ya 100 kushiriki, wamo Mwana FA, Juma Nature, Dullah Makabila, Gigy Money, Vitalis Maembe
>>Pia wapo Mashauzi Classic, Malkia Khadija Kopa, Msondo Ngoma, Sisi Tambala, Sinaubi Zawose
NA MWANDISHI WETU
TAMASHA la 38 la Sanaa Bagamoyo linaanza rasmi kesho Oktoba 19-26 katika mji wa kihistoria Bagamoyo mkoani Pwani litatemesha mji wa Bagamoyo na mkoa wa Pwani kwa ujumla.
Mwaka huu tamasha hilo litaanza kwa mtindo wa tofauti na ilivyozoeleka, litaanza kwa kuzunguka mitaa mbalimbali ya wilaya hiyo, lengo likiwa ni hamasa kwa tukio hilo muhimu.
Wasanii wa kazi mbalimbali watazunguka mji huo kwa ngoma mbalimbali ili kuwachochea wadau kujitokeza katika ukumbi ulioko chuoni hapo.
Zoezi hilo la kuzunguka maeneo ya Bagamoyo, litaanza asubuhi likishirikisha wadau mbalimbali.
Bagamoyo ni mojawapo ya maeneo yenye urithi na utajiri mkubwa wa kiutamaduni Ulimwenguni, ambako Tamasha hilo la kimataifa, kwa mara nyingine tena litawakutanisha wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, ambao wataonesha kazi zao za sanaa na utamaduni.
Dk. Hebert Makoye, ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), ambao ni waandaaji wa tamasha hilo linalozidi kujizolea umaarufu kila mwaka, anasema lengo ni kuendeleza na kudumisha Utamaduni wa Mtanzania, kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa mataifa mengine kupitia warsha, kongamano na maonyesho mbalimbali.
Dk. Makoye, anasema tamasha la 38 linatarajiwa kushirikisha wasanii zaidi ya 100 ya hapa nchini na nje, likiwa na dhamira ya kubadilishana uzoefu katika sanaa, hivyo ni nafasi ya wadau mbalimbali wa sanaa kujitokeza na kushuhudia elimu kutoka kwa wasanii watakaopanda jukwaani.
Anasema, tamasha la mwaka huu litashirikisha vijana wa shule za Msingi na Sekondari kutoka Bagamoyo, Vyuo na Vyuo Vikuu.
“Mwaka huu, tamasha linatarajiwa kuhudhuriwa na jumla ya watazamaji 60,000 kutoka maeneo ya Bagamoyo, Dar es Salaam na sehemu zingine za Tanzania pamoja na nje ya nchi,” anasema Dk. Makoye na kuongeza.
Kusudi la Tamasha hili ni kutoa fursa kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi, pamoja na watazamaji kukutana na kuuenzi utajiri wa utamaduni wao unaowatofautisha na mataifa mengine, ambao unaonyesha utofauti wao katika muktadha wa maadili na mshikamano, pamoja na ubunifu.
Malengo maalum ya Tamasha
Dk. Makoye, anasema ni jukwaa kwa wanafunzi wa TaSUBa na wa kutoka taasisi zingine za mafunzo, kuonesha kazi zao na stadi walizopata katika mafunzo yao ya sanaa na utamaduni.
Anasema, pia ni kukuza na kubadilishana tamaduni kati ya wasanii wa ndani na wa kimataifa, ni jukwaa la wasanii wachanga kuonesha vipaji na ustadi wao kwenye sanaa na utamaduni, kuongeza uhamasishaji miongoni mwa vijana na wasanii juu ya masuala yanayohusu sanaa, michezo na utamaduni wa Kitanzania.
Dk. Makoye, anasema Kauli mbiu ya Tamasha la mwaka huu ni ‘Sanaa na Utamaduni Ajira Yangu’.
Aidha, anasema katika tamasha la mwaka huu, kutakuwa na maonesho ya bidhaa mbalimbali za sanaa na za kiutamaduni, vyakula mbalimbali kama vile nyama choma, samaki, pamoja na vyakula vya baharini.
Pia, anasema wageni watapata fursa ya kutembelea mji wa kihistoria wa Bagamoyo.
TaSUBa, Clouds Plus kuboresha tamasha
Mapema mwaka huu, TaSUBa imeingia makubaliano na Kampuni ya Clouds Plus Production yenye lengo la kushirikiana katika kusaka rasilimali za uendeshaji wa Tamasha hilo la Kimataifa la 38.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano iliyofanyika ukumbi mkubwa wa maonesho wa TaSUBa, Dk. Makoye, anasema lengo kuu la makubaliano hayo ni kutafuta rasilimali zitazowezesha kuendesha tamasha hilo lenye lengo la kuenzi, kudumisha na kutunza utamaduni wa Mtanzania.
Anasema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1982, tamasha limekuwa likifanyika kila mwaka bila kukosa mbali na kukumbwa na uhaba wa fedha, lakini anaamini kwa kushirikiana na kampuni kubwa ya biashara ya Clouds Plus Production, tamasha linaweza kuvutia wawekezaji mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Uendeshaji wa Clouds Plus Production, Ramadhani Bukini, anasema kampuni yake inayomiliki runinga na redio, itatumia mbinu mbalimbali kulitangaza tamasha hilo Duniani ili kufanya lifikie malengo yake ya kuenzi na kudumisha utamaduni wa Mtanzania na pia kuvutia wawekezaji wengi.
Ratiba mahsusi
Dk. Makoye, anasema katika wiki ya tamasha zipo siku zitakuwa maalum kwa ajili ya ratiba mahsusi, ambako Jumatatu itakuwa ni ‘Usiku wa Filamu’, Jumatano ‘Usiku wa Muziki wa Dansi’ na Jumapili ‘Usiku wa Taarabu’.
Wasanii wanaotarajiwa kupanda jukwaani
Wasanii wanaotarajiwa kupanda jukwaani mwaka huu ni Khamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, Juma Kassim ‘Juma Nature’, Barnaba Elias ‘Barnaba’, Dullah Makabila, Gigy Money na Vitalis Maembe.
Wengine ni Mashauzi Classic, Malkia Khadija Kopa, Thabit Abdul, Bendi ya Msondo Ngoma, John Kitime na bendi yake, Sisi Tambala, Sinaubi Zawose, Shada Acrobatics na Baldreda kutoka Marekani.
Dk. Makoye, anabainisha kuwa pia makundi ya hapa nchini yatashiriki, ambapo Bagamoyo itatoa 37, Dar es Salaam 28, Zanzibar mawili huku mikoa ya Mwanza, Ruvuma, Morogoro, Kilimanjaro, Njombe yatatoa kundi moja moja, Arusha mawili na Dodoma 10.
Makundi kutoka nje ya Tanzania, Marekani yatakuwa mawili, Botswana, Korea Kusini, Zimbabwe, Uganda, Zambia na Finland kundi moja moja huku kutoka Kenya yakiwa nane.
Mgeni rasmi ufunguzi/ufungaji
Dk. Makoye, anaweka wazi mgeni rasmi wakati wa ufunguzi katika tamasha la mwaka huu, anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe huku wakati wa kufunga atakuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juliana Shonza.