Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(wa pili kulia aliyekaa) akisikiliza jambo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama( aliyesimama), kushoto aliyekaa ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Amour Juma wakati wa kuzindua na kuwasha umeme katika Kijiji cha Mpiji, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha,mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( wa pili kulia) akikata utepe kuashiria kuzindua na kuwasha umeme katika moja ya nyumba za Kijiji cha Mpiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha,kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Amour Jumaa, na wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( aliyesimama),akizungumza na wakazi wa Misugusugu baada ya kupata malalamiko kuwa baadhi ya kaya zimerukwa na mradi wa usambazji umeme vijiji, hata hivyo amewahakikishia wananchi hao kuwa wote watapata umeme, kulia aliyekaa ni Mbunge wa Kibaha mjini, Silvestry Koka
……………….
Na Zuena Msuya , Pwani
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Nchini(TANESCO)kutoa taarifa za utekelezaji wa Miradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini kwa viongozi wa vijiji pamoja na wananchi wa maeneo husika ili wafahamu hatua zaidi za utekelezaji wa miradi hiyo.
Mgalu alisema hayo kwa nyakati tofauti, Oktoba 16, 2019 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuzindua na kuwasha Umeme katika Kijiji cha Mpiji, Kata Boko katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji Umeme katika vijiji vya Kiluvya, Misugusugu, Mkombozi pamoja na katika Mtaa wa Mwambisi wilayani humo.
Aidha Mgalu alisema, kuwa TANESCO wakiweka utaratibu wa kuzungumza na Viongozi wa Vijiji pamoja na wananchi mara kwa mara juu ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi husika ,kutaondoa maswali mengi pamoja na wasiwasi walionao wananchi dhidi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa usambazaji wa umeme.
“Unajua watanzania ni waelewa sana,unapompa mtu taarifa ya kile kinachofanyika katika eneo lake kwa wakati sahihi inamfanya awe na amani na wale waliopewa dhamana ya kutekeleza jambo husika, pia kuendelea kuiamini serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake, na hii itawaondolea hofu na maswali mengi wananchi, sasa msipofanya hivyo, wao watajuaje kinachoendelea katika maeneo yao!? Tanesco waelezeni wananchi kila hatua inayofikiwa katika kutekeleza miradi ya umeme”, alisisitiza Mgalu.
Vilevile alitumia ziara hiyo kuwaeleza watanzania ambao bado hawajafikiwa na miradi ya usambazaji wa umeme kuwa na subira wakati serikali inaendelea kutekeleza kazi hiyo kwa awamu, kwa kuwa si jambo jepesi kuwafikia wananchi wote kwa siku moja.
Aliweka wazi kuwa lengo la serikali ni kufikisha huduma ya umeme kwa kila mtanzania, na kueleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Vijiji 2018 tu, ndiyo vilikuwa na umeme, sasa hivi idadi imeongezeka na kufikia zaidi ya vijiji 8100 na tayari zaidi ya vijiji 6000 vimeunganishwa, lengo ni kuvifikia vijiji vyote 12,319 nchi nzima ikifikapo mwezi Juni ,2021.
“ Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mingi na muhimu katika kila sekta, kuna miradi ya Afya, Elimu, Barabara, Maji na kadhalika, hii yote inahitaji fedha nyingi na iwafikie wananchi wote na kwa wakati, serikali yetu ni sikivu na inatekeleza haya yote kwa kwa wananchi wake, hivyo fedha inayopatika inagawanywa katika kila sekta ili kutekeleza huduma zote muhimu kwa awamu kadri fedha inavyopatikana, hivyo wale ambao bado hamjafikiwa kuweni na subira, lengo ni kuwapatia wananchi wote huduma bora”, alisema Mgalu.
Mgalu alieleza kuwa, mkandarasi wa kampuni ya Sengerema amefikia 90% ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme katika vijijini vyote vya Wilaya ya Kibaha,kazi kubwa aliyonayo sasa ni kuwasha vijiji hivyo hadi mwezi Desemba 2019,kisha kuangalia mapungufu yalipo na kuyafanyia kazi, ili ifikapo mwezi Juni 2020 awe amemaliza mradi huo na kuukamilisha kwa wakati.
Aliendelea kumsihi mkandarasi huyo kuongeza kasi ya kuwaunganisha wateja ambao tayari wamelepia huduma hiyo, sambamba na hilo aliwahimiza wananchi kulipia haraka gharama za kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu.
Serikali ilitenga zaidi ya shilingi Bilioni 17, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini katika Mkoa wa Pwani, pia iliongeza shilingi Bilioni 14 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Peri Urban katika Wilaya ya Kibaha pekee, vilevile kupitia mapato ya ndani ya TANESCO, miradi ya usambazaji umeme 11 itatekelezwa katika wilaya hiyo kutokana kuwepo kwa mahitaji makubwa ya umeme katika wilaya hiyo yanayosababishwa na uwepo wa viwanda.
Aidha katika mazungumzo yake na wakazi wa Kijiji cha Misugusugu,aliitaka TANESCO kuwafungia Transfoma inayokidhi mahitaji ya umeme katika kijiji hicho na maeneo yanayowazunguka ili kuondoa adha ya kukatika umeme katika eneo hilo mara kwa mara ambayo inasababishwa na kulemewa kwa transfoma iliyopo.
Hata hivyo aliwaagiza watendaji wa TANESCO kufanya uchunguzi upya kubaini kaya za maeneo ya kijiji cha Misugusugu zilizoachwa katika awamu zilizotangulia ili na wao wapate umeme katika awamu zijazo kwa kuwa zoezi la kusambza umeme vijijini na kuwaunganisha wateja ni endelevu kwa kuwa kila siku mahitaji ya umeme yanaongezeka nchini.