Baadhi ya wananchi wa vijiji vya Mrito na Kibaso katika tarafa ya Ingwe wilaya ya Tarime mkoa wa mara wakinyoosha mikono kuunga mkono jitihada za Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Mendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwenda kutatua mgogoro wa takriban miaka 29 kati ya vijiji hivyo jana.
Mwananchi wa kijiji cha Mrito wilaya ya Tarime Raphael Mwita akimkabidhi nyaraka Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa muda mefu kati ya vijiji vya Mrito na Kibaso mkoani jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na timu iliyoteuliwa na pande zenye mgogoro wa mpaka kati ya vijiji vya Mrito na Kibaso wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wakati wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya vijiji hivyo jana (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
…………………….
Na Munir Shemweta, WANMM TARIME
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza timu ya Wataalamu wa sekta ya ardhi iende katika tarafa ya Ingwe wilaya ya Tarime mkoa wa Mara kwenda kubainisha mipaka ya kiutawala kwa ajili ya kutatua mgogoro wa muda mrefu wa mipaka baina ya kijiji cha Mrito na Kibaso.
Uamuzi huo Dkt Mabula unafuatia jitihada za kutafuta suluhu ya mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili kukwama kutokana na kila upande kudai sehemu ya eneo la kijiji cha Mrito liko upande wake.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, timu hiyo itahusisha wataalamu wa sekta hiyo kutoka ofisi ya Ardhi Kanda ya Simuyu na wale wa ofisi ya mkoa wa Mara badala ya Tarime kufuatia baadhi yao kutuhumiwa na pande hizo kuwa wamekuwa wakichangia kuendelea kwa mgogoro baina ya vijiji hivyo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alishangazwa kusikia kutoka kwa wananchi wa vijiji vya Mrito na Kibaso kuwa ndani ya kijiji kimoja kuna viongozi wawili wa kijiji jambo alilolieleza kuwa suala hilo halikubaliki.
Dkt Mabula alibainisha kwa kusema kuwa, zoezi hilo litakalohusisha pia wananchi kumi kutoka kila upande wa vijiji vyenye mgogoro litafanyika kwa muda wa siku mbili na kusisitiza kuwa lengo ni kumaliza kabisa mgogoro huo uliodumu kwa takriban miaka 29.
Alisema, baada ya kukamilika kwa zoezi la kubainisha mipaka ya kiutawala taarifa yake itawasilishwa kwa mkuu wa wilaya ya Tarime mkoani Mara Mtemi Msafiri ambaye jumanne ijayo tarehe 22 Oktoba 2019 atatakiwa kuwaeleza wananchi wa vijiji hivyo makubaliana yatakayofikiwa kwa nia ya kumaliza mgogoro huo.
Awali kulikuwa na mabishano makali ya pande zinazopingana katika mgogoro huo ambapo wananchi wa kijiji cha Mrito walidai wenzao wa Kibaso wamevamia eneo lao huku wale wa Kibaso wakidai sehemua ya eneo linalodaiwa ni la Mrito ni la kwao.
Joseph Mangure aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Mrito tangu mwaka 2009 hadi 2014 alisema sehemu ya eneo la kijiji cha Mrito inayodaiwa na wananchi wa Kibaso kuwa ni la kwao siyo sahihi kwa kuwa kijiji cha Mrito kina nyaraka zote zinazoonesha mipaka yake tofauti na wananchi wa Kibaso alioeleza kuwa hawana Nyaraka zinazoonesha uhalali wa eneo lake.
Naye Diwani wa Kata ya Bihanja wilayani Tarime Mustafa Masiani alieleza kuwa suluhu pekee ya mgogoro baina ya vijiji hivyo ni kwa viongozi wa serikali za vijji husika kukaa pamoja na na kutafuta suluhu ya mgogoro na kubainisha kuwa tatizo lililopo ni baadhi ya wananchi kuufanya uongozi wa vijiji kama uongozi wa Koo.