Baadhi ya wanawake na wananchi wa Kijiji cha Gehandu wakifuatilia hotuba na salamu mbalimbali za viongozi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini yaliyofanyika katika Wilaya ha Hanang mkoani Manyara.
…………………
Picha zote na Kitengo cha Mawasilino WAMJW
Na Mwandishi Wetu Hanang Manyara
Wanawake waishio katika Kijiji cha Gehandu wameiomba Serikali kutatua changamoto za Wanawake waishio kijijini hapo ikiwemo uhaba wa maji yanayopatikana umbali wa Kilometa 30 na ukamilishaji wa jengo la Kituo cha Afya litakaosaidia kutatua upatikanaji wa huduma za Afya.
Wakizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini wanawake wa Kijiji cha Gehandu mmoja wa Mwanamke Bi. Ate Giegon amesema kuwa wanawake wa kijiji hicho wanakabiliwa na tatizo la kutafuta maji kwa umbali mrefu ambayo ni changamoto kubwa kwani husababisha kusimama kwa shughuli nyingine za kiuchumi.
Ameongeza kuwa wanaume wamekuwa wakiwakandamiza wanawake kwa kuwaachia kushugulika na shughuli zote za nyumbani na za kiuchumi.
“Wanaume hawana mchango wowote kwetu bali wamekuwa wakitukandamiza na kuturudisha nyuma katika maendeleo”alisema Bi. Ate
Bi. Ate ameiomba Serikali kutoa elimu kwa wanaume kuachana na vitendo vya ukatili na ukandamizaji kwa wanawake hasa wale waishio vijijini kwani kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakirudisha nyuma kimaendeleo.
Naye Bi Happy Gwarugwa ameeleza kuwa njia pekee ya kumkomboa mwanamke ni kumuelimisha kwa kumpatia elimu itakayomsaidia kupambanua fursa zilizopo zikamsaidia kujikwamua kiuchumi na kuindeleza familia na taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa wanawake waliofanikiwa kupata elimu wasidie wanawake wenzao hasa waishio vijijini kupata elimu ya kutambua haki zao ambazo zinakandamizwa na wanaume kwa asilimia kubwa.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang Bw. Brayson Kibasa amesema kuwa Wilaya imejipanga katika kutatua changamoto za wananchi wa kijiji cha Gehandu haswa wanawake kwa kuhakikisha wanatekelza miradi ya maji itakayosaidia kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji kijijini hapo.
Bw. Kibasa ameongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang inajipanga kuhakikisha Boma la Kituo cha Afya lililojengwa kwa nguvu za wananchi linamalizika ili kuwezesha upatikananji wa huduma za Afya hasa huduma ya Mama na Mtoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Julius Mbilinyi ameeleza kuwa Maadhimisho haya yanalenga kuwawezesha wanawake wanaoishi vijijini kutatua changamoto zinazowakabili wanawake wanaoishi kijijini kupitia rasilimali zinazowazunguka.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha Mwanamke hasa aishie kijijini kuondoka na vitendo vya ukatili amesema Wizara iimeanzisha na kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto ambao unaeleza jinsi Jamii na Serikali inavyotekeleza wajibu wao katika kumlinda Mwanamke na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Akiwahutubia Wananchi wa Kijiji cha Gehandu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Elizabeth Kitundu ameiagiza Halmshauri ya Wilaya ya Hanang kuhakikisha changamoto zilizotolewa na wanawake wa kijiji cha Hanang zinapatiwa ufumbuzi na haswa suala la upatikanaji wa maji na huduma za Afya.
Aidha ametoa rai kwa wadau kuwawezesha wanawake wanaoishi kijijini ili waweze kujitegemea na kujiamini na hata kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kupunguza changamoto zinazowakabili.
Ameongeza kuwa wanawake hawana sababu ya kuogopa kujitokeza katika jamii kusimama na kupigania haki zao kwani italeta nguvu ikiwa wanawake wataungana pamoja kutetea haki zao.
Ameitaka jamii ya Mkoa wa Manyara kuachana na mila zisizofaa hasa vitendo vya ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni zinazosababisha kukatiza ndoto za watoto wengi wa kike nchini.
Aidha Afisa kutoka Dawati la Polisi la Jinsia na Watoto Mkoa wa Manyara Pili Serieli amesema kuwa Mwanamke na Mtoto ndio waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili hivyo jamii inatakiwa kuripoti vitendo vya kikatili ili kumsaidia Mwanamke na mtoto na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Ameongeza kuwa wananchi hawana haja ya kukata tamaa endapo mtuhumiwa akiwa ameachiwa huru kwa dhamana bali waendelee kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili kwani Jeshi la Polisi linaendelea kupambana na vitendo vya ukatili.