Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kata ya Kijungu Wilayani Kiteto.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kata ya Lengatei Wilayani Kiteto.
Wananchi wa Kata ya Dongo Wilayani Kiteto, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti alipotembea eneo hilo.
…………………
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti ameunguruma Wilayani Kiteto kwa kuagiza wakulima waheshimu eneo la malisho la wafugaji wa Amei na wakulima wa Kata ya Dongo walionyang’anywa maeneo yao warudishiwe kwani hawakupewa eneo mbadala.
Mnyeti alitoa maagizo hayo Wilayani Kiteto alipotembelea maeneo hayo kwenye ziara yake ya siku tano ya wilaya ya Kiteto.
Alisema wakulima wa Amei wasiingilie eneo la mifugo kwani limewekwa kwa ajili ya wafugaji.
“Mlishajipangia wenyewe kuwa lile ni eneo la mifugo hivyo wakulima muache kusogelea hapo mtasababisha vurugu ili hali mlijiamulia wenyewe matumizi ya ardhi yenu,” alisema Mnyeti.
Alisema kwenye eneo la Dongo kuna baadhi ya wakulima walifukuzwa kwenye sehemu yao bila kupewa eneo mbadala hivyo warudi katika eneo lao.
“Wakulima walifukuzwa bila kupewa eneo lingine hivyo rudini ili muendeshe maisha yenu kama ilivyokuwa awali kwani hamkupewa maeneo mbadala ya kulima,” alisema Mnyeti.
Pia, aliwataka wafugaji na wakulima kuheshimu mipango ya matumizi bora ya ardhi waliyojiwekea ili kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
“Heshimuni mpango huo mlioamua wenyewe kwani mfugaji akiheshimu sehemu ya wakulima na wakulima wakiheshimu eneo la wafugaji hakutatokea tatizo lolote,” alisema Mnyeti.
Mkuu huyo wa mkoa alileta faraja kwa mkazi wa kijiji cha Zambia kikongwe aliyenyang’anywa eneo na baadhi ya viongozi wa kijiji hicho.
“Kuanzia sasa hivi wewe mama rudi kwenye eneo lake la awali na mtu yeyote asikusumbue mtendaji wa kijiji, kata na ofisa Tarafa mlindeni huyu mama asiguswe na mtu,” alisema Mnyeti.
Akiwa kwenye kata ya Lengatei aliagiza mkazi wa eneo hilo Hassan Ramadhan kurudishiwa eneo lake lililotaka kujengwa shule shikizi ili hali alishinda shauri lake kwenye baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Kiteto.
Lengo la ziara hiyo ni kuzungumza na wananchi, kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero na changamoto na kuyapatia majawabu na kuhamasisha wananchi kujiandikisha ili waweze kupiga kura ya kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa.