Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa maabara unaoendelea katika shule ya Sekondari Janda iliyoko wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia ramani ya ujenzi wa shule ya msingi ya mfano Bwega iliyoko wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akitoa maelekezo mara baada ya kukagua ujenzi wa mabweni ya shule sekondari Muyama iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akionesha dosari kwenye jengo la maabara la shule ya sekondari Janda wakati akikagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika shule hiyo
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua moja ya dawati lililoko katika Shule ya Sekondari Muyama mara baada ya kukagua ujenzi wa darasa hilo
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza na wanafunzi katika shule ya sekondari Janda iliyopo Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma mara baada ya kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa shuleni hapo
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akikagua moja ya nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Kasumo iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma
……………………..
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameonesha kukerwa na usimamizi mbovu wa miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara anayoisimamia, Dkt. Leonard Akwilapo kuleta wataalamu watakaofanya ukaguzi maalum wa utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya hiyo.
Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma mara baada ya kukagua baadhi ya miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)na kubaini uwepo wa kasoro kadhaa ikiwemo matumizi ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya Kiwango na majengo ya shule ya Msingi ya mfano Bwega kutofautiana na ramani iliyopendekezwa na wizara .
“Kwa ujumla usimamizi wa Miradi katika wilaya ya Buhigwe siyo mzuri, maafisa elimu hawawajibiki katika kuangalia kazi zao, unakuta kazi zimefanyika hovyo, watu hawafuatilii,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri Ndalichako amesema Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hatimizi wajibu wake ipasavyo kwa kuwa ameshindwa kusimamia miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa na kuruhusu matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora lakini pia ameshindwa kufuata ramani katika ujenzi wa majengo ya shule ya msingi ya mfano inayojengwa wilayani humo.
Kiongozi huyo amesema tayari amewasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Leonard Akwilapo ili ufanyike ukaguzi wa kina katika miradi ya elimu Wilaya ya Buhigwe lengo likiwa ni kubaini mapungufu na iwapo kuna mtu kafanya uzembe kwa manufaa yake awajibike.
“Inabidi kabla ya kuleta fedha nyingine za miradi ya elimu wilayani Buhigwe ije timu ya watalaamu mainjinia wachunguze walinganishe BoQ na kilichofanyika, haiwezekani turuhusu uzembe kama huu kuendelea kwenye miradi inayotumia fedha ya wananchi wanyonge,” aliongeza Waziri Ndalichako.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayanalina amemshukuru Waziri Ndalichako kwa ziara yake wilayani humo na kusema kuwa mapungufu yote yaliyobainika tayari Kamati yake imeyatolea maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na kwamba zoezi linaloendelea ni kuwachukulia hatua wahusika.
“Kamati ya Usalama ya wilaya ilibaini mapungufu katika miradi mbalimbali na tulitoa maelekezo kupitia kwa Mkurugenzi na vyombo vyetu vilishaagizwa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki,” amesema Mkuu wa Wilaya hiyo, Ngayalina.
Naye mMkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Anosta Nyamoga amesema ofisi yake tayari imemfukuza kazi fundi aliyekuwa na mkataba wa kufanya ukarabati na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Janda kutokana na kufanya kazi hiyo chini ya viwango na kuahidi kuzifanyia kazi kasoro zote ambazo zimebainishwa na Waziri Ndalichako.
Akiwa wilayani Buhigwe Waziri Ndalichako amekagua miradi ya elimu katika shule ya msingi Bwega, shule ya sekondari Janda, shule ya sekondari Muyama na shule ya msingi Kasumo ambayo kwa pamoja inatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.
Waziri Ndalichako yuko Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na Halmashauri ya Mji Kasulu.