NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MRATIBU wa huduma za chanjo mkoani Pwani ,Abbas Hincha amesisitiza ni haki ya mtoto kupata chanjo na amewaasa baadhi ya watu kuacha kupotosha kuwa chanjo inayotolewa kwaajili ya surua na surua rubella inaua nguvu za kiume na uzazi ukubwani mwao.
Aidha ameeleza ,mkoa huo unatarajia kufikia watoto 165.875 wenye umri uanzia miezi Tisa hadi chini ya miaka mitano katika kampeni ya chanjo ya magonjwa ya Surua Rubella itakayoanza Octoba 17 -21 mwaka huu.
Mratibu wa chanjo mkoani Pwani, Abbas Hincha alieleza hayo ,wakati akizungumza na waandishi wa habari katika semina ya afya ya msingi kwa ajili ya kampeni ya kitaifa ya chanjo ya Surua Rubella na Polio ya Sindano.
Alisema chanjo hiyo ni muhimu kwa afya ya mtoto na mtoto asiyekamilisha ratiba ya chanjo ni hatari katika maisha yake na jamii inayomzunguka kwani ni rahisi kuambukizwa magonjwa na kuambukiza wengine.
Pamoja na hilo, kampeni hiyo itahusisha utoaji wa chanjo ya polio ya sindano kwa watoto wapatao 93,546 wenye umri wa mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu na nusu kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo.
“Lengo kuu la kitaifa ni kufikia zaidi ya asilimia 99 ya watoto waliolengwa kupata chanjo hizo katika kila eneo na ngazi zote ambapo mkoa umetenga jumla ya timu 156 za uchanjaji ili kufikia vituo 553 vilivyoainishwa na halmashauri zote na maeneo 245 ambayo ni magumu kufikika kutokana na sababu mbalimbali”alifafanua Hincha.
Hincha alisema, hadi sasa mkoa umepokea na kusambaza chanjo katika halmashauri zote na usambazaji ngazi ya vituo unaendelea.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo alifafanua, kiwango cha Surua Rubella kimeendelea kuwa juu ,kwa mkoa ni zaidi ya asilimia 100 idadi ya watoto wasiokamilisha chanjo na wasiochanjwa hali ambayo inaweza ikasababisha mlipuko wa ugonjwa wa surua.
Alibainisha ,Rubella ni dada wa surua unatoka vipele vidogo vidogo na mama mjamzito akipata mtoto huathirika zaidi.
Ndikilo alitaja madhara yatokanayo na ugonjwa wa surua kuwa ni ,masikio kutoa usaha,,vidonda vya macho ambao husababisha upofu,Nimonia,utapiamlo ,kuvimba ubongo na kifo.